AFCON 2019 Tupogo!
Vodacom Data Datani!

Sakata la Spika Ndugai na CAG, Zitto Kabwe alipeleka kwa Mkuu wa Umoja wa Mabunge ya Jumuiya ya Madola (+video)

Mbunge wa Kigoma Mjini, Mhe. Zitto Kabwe ameingilia kati sakata la Spika wa Bunge la Jamhuri ya Tanzania, Mhe. Job Ndugai na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali nchini (CAG), Prof. Musa Assad kwa kulipelekwa kwa Mkuu wa Umoja wa Mabunge ya Jumuiya ya Madola (CPA).

Zitto Kabwe amesema hayo leo Jumapili Januari 13, 2019 kwenye mkutano wake na Waandishi wa Habari.

SOMA TAARIFA YAKE KAMILI HAPA CHINI

Mtakumbuka kuwa mnamo Januari 9, 2019 niliandika Barua kwa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mabunge ya Jumuiya ya Madola (CPA), Mheshimiwa Akbar Khan nikimuarifu kuhusu sokomoko lililoibuka nchini mwetu, kutokana na hatua ya Spika wa Bunge letu la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Job Justino Ndugai kumuagiza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali nchini (CAG), Profesa Mussa Juma Assad aripoti kwenye Kamati ya Maadili ya Bunge kuhojiwa.

Siku hiyo hiyo ya Januari 9, Mheshimiwa Job Yustino Ndugai alijibu Barua yangu hiyo kwa kumwandikia Katibu Mkuu wa Umoja wa Mabunge ya Jumuiya ya Madola kuwa suala hilo ni suala la ndani ya nchi, na kwamba CPA hawapaswi kuliingilia.

Aidha katika barua yake ya majibu Spika Ndugai, ambaye amekuwa na heshima kubwa katika jumuiya ya wanaCPA duniani, alikiri kuwa ni kweli kitendo alichofanya (cha kumpeleka CAG akahojiwe kwenye Kamati ya Maadili ya Bunge) hakijawahi kufanywa na Spika wa Bunge lolote ndani ya Jumuiya ya Madola, lakini akajitetea kuwa pia kuwa katika nchi za Jumuiya ya Madola haijapata kutokea Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Mahesabu kulivunjia heshima Bunge.

Utetezi huu wa Spika si sahihi, alichokieleza si jambo la kweli. Mwaka 2015, CAG wa nchi jirani yetu ya Uganda, Mheshimiwa John F. S. Muwanga alilisema hadharani Bunge la Uganda kwa kutofanya Kazi yake sawa sawa (Kama alivyofanya Profesa Assad), lakini Spika wa Bunge la Uganda, mheshimiwa Rebecca Alitwala Kadaga hakuchukua hatua alizochokua Spika wa Bunge la Tanzania, Mheshimiwa Job Ndugai, za kumpeleka CAG wao akahojiwe kwenye Bunge la Uganda kwa tuhuma za kudhalilisha Bunge.

Nafurahi kuwaarifu kuwa, Umoja wa Mabunge ya Nchi za Jumuiya ya Masala (CPA) umeamua kufuatilia jambo hili, ili kuhakikisha kuwa linaisha bila kuathiri Uhuru wa Kikatiba na Kisheria wa Ofisi ya CAG.

Jana nimepokea Barua kutoka kwa Katibu Mkuu wa CPA ikiniarifu kuwa Katibu Mkuu huyo amelifikisha jambo hili kwa Mwenyekiti wa CPA na Spika wa Bunge la Cameroon Mheshimiwa Emilia Lifaka ili aweze kushauriana na Spika wa Tanzania namna bora ya kushughulikia migongano Kati ya Bunge na CAG.

Nimetiwa moyo na hatua hiyo ya CPA kufanyia Kazi jambo hili kwa haraka na kazi inayostahili, na ni Imani yangu kuwa Spika wa Bunge letu, Mheshimiwa Ndugai atazingatia heshima aliyojijengea Katika Mabunge ya CPA na kuepuka kuingia Katika rekodi mbaya kabisa Katika historia ya zaidi ya miaka 100 ya Mabunge ya Jumuiya ya Madola. Nitaendelea kuwajuza maendeleo ya usuluhishi huu wa CPA juu ya jambo hili kila nipatapo taarifa mpya.

B: Tunafungua Kesi Mahakama Kuu

Napenda pia kuwajulisha kuwa kutokana na uzito wa jambo hili haswa Katika kulinda misingi ya Katiba ya nchi yetu ya Uhuru wa maoni na Kinga ya Kikatiba ya CAG, wabunge wanne wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania tumeamua kufungua kesi ya Kikatiba Mahakama Kuu ya Tanzania, Masjala ya Dar es Salaam ili Mahakama itupe tafsiri ya Kisheria juu ya mipaka ya Kinga ya CAG pamoja na mamlaka ya Spika wa Bunge kuweza kumshtaki mwananchi bila kuathiri Uhuru wa maoni kikatiba.

Wabunge tulioamua kufungua kesi hiyo ni wafuatao/

  1. Kabwe Zuberi Ruyagwa Kabwe – Kigoma Mjini
  2. Saed Ahmed Kubenea – Ubungo
  3. Salome Wycllife Makamba – Viti Maalumu
  4. Hamidu Hassan Bobali – Mchinga
  5. Anthony Calist Komu – Moshi Vijijini

Tunapenda ifahamike kwa Umma kuwa sisi hatumtetei Prof. Mussa Juma Assad, bali tunatetea HESHIMA na UHURU wa Ofisi ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (NAOT), tunaamini kuwa hatua hii aliyochukua Spika Ndugai ikiachwa itaweka msingi (Precedence) mbaya wa CAG kuingiliwa uhuru wake na taasisi mbalimbali kinyume na Katiba.

Sisi wabunge wanne, kupitia kwa Wakili wetu, ndugu Fatma Karume, tunaiomba Mahakama itoe tafsiri ya Kinga ya CAG iliyopo kikatiba, itoe tafsiri ya Sheria ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge Katika kushtaki watu wanaosemekana kudharau Bunge;

i. Tukihoji Mahakamani mamlaka ya Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuweza kumuita mtu yeyote kuhojiwa kwenye Kamati ya Maadili ya Bunge bila Azimio la Bunge zima.

ii. Tukiiomba Mahakama Kuu imzuie Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali wa Tanzania, CAG kuitika wito wa Spika.

iii. Na tukiomba Mahakama Kuu imkataze Spika kutekeleza wito wake kwa Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali CAG, kwa kuwa ni kinyume na Katiba.

Tumemwagiza Wakili wetu kuisajili kesi hii chini ya hati ya dharura, na tunaiomba mahakama itazame jambo hili kwa muktadha mpana, kwani ni kesi yenye maslahi makubwa kwa umma, na madhara yake ni kwamba jambo hili likiachwa ipo siku pia Jaji Mkuu anaweza kuitwa mbele ya Kamati ya Haki, Kinga na Madaraka ya Bunge kwa maoni yake kutokumpendeza Spika.

Mara baada ya taratibu za mahakama kukamilika tutawapa taarifa ya hatua mbalimbali za kesi hii.

Nawashukuru sana

Kabwe Z. Ruyagwa Zitto
Kiongozi wa Chama, ACT Wazalendo
Mbunge – Kigoma Mjini
Januari 13, 2019
Dar es Salaam

Related Articles

Back to top button
Bongo5

FREE
VIEW