Habari

Samatta: Mahakama haina uhuru kwa Bunge

JAJI Mkuu mstaafu, Bw. Barnabas Samatta, ambaye ameanza rasmi maisha ya ustaafu baada ya kuitumikia Serikali ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania katika nyadhifa mbalimbali kwa miaka takribani 31, amesema moja ya mambo yaliyowahi uamuzi mbalimbali wa Idara hiyo.



Na Hassan Abbas


JAJI Mkuu mstaafu, Bw. Barnabas Samatta, ambaye ameanza rasmi maisha ya ustaafu baada ya kuitumikia Serikali ya Jamhuri ya Muungano ya Tanzania katika nyadhifa mbalimbali kwa miaka takribani 31, amesema moja ya mambo yaliyowahi uamuzi mbalimbali wa Idara hiyo.


Jaji Samatta alizungumzia suala hilo na pia kutoa wosia wake katika masuala mengine kadhaa ya kitaifa, alipofanya mahojiano maalumu na gazeti hili jana nyumbani kwake, Oysterbay, Dar es Salaam.


Jaji Samatta alitamka bayana kuwa Bunge lina mipaka katika utungaji sheria, alipokuwa akijibu swali kuhusu mtazamo wake juu ya vitendo vya mara kadhaa vilivyofanywa na Bunge kufuta uamuzi wa Mahakama kwa kutotekeleza hukumu zake na badala yake kutunga sheria mpya, na mara kadhaa kuibadili Katiba ya nchi.


Moja ya uamuzi ambao unalalamikiwa na wafuatiliaji wa masuala ya sheria na siasa nchini ni wa kesi namba 5 ya mwaka 1995 ambapo Jaji Kahwa Lugakingira, alihukumu kuwa wagombea binafsi ni halali kushiriki katika chaguzi mbalimbali ukiwamo urais.


Badala ya kupinga uamuzi huo kwa kufungua kesi Mahakama ya Rufani, Serikali ilipeleka muswada bungeni na kubadili Katiba katika ibara ya 39 kwa kuongeza kipengele kilichoeleza, kuwa moja ya sifa ya mtu kugombea uongozi wa kisiasa ni kuwa mwanachama wa chama cha siasa, mabadiliko ambayo moja kwa moja yaliifanya hukumu ya Jaji Lugakingira kuwa haina maana tena.


Akizungumzia hali hiyo na matukio mengine ya Bunge kufuta uamuzi wa Mahakama, Bw. Samatta alisema: “Tunashukuru kuwa hivi sasa Katiba iko wazi zaidi kuhusu majukumu ya mihimili mitatu ya Dola.


“Bunge lina kazi ya kutunga sheria na linachotakiwa kufanya ni kufanya mabadiliko tu ya sheria kwa kadri hukumu ya Mahakama ilivyoelekeza na si kufuta uamuzi wa Mahakama.”


Akifafanua kuhusu mamlaka ya Bunge kutunga sheria na hasa kubadili Katiba ya nchi, Bw. Samatta alisema kwa mtazamo wake, Bunge halipaswi kubadili Katiba kiholela, bali linapaswa kufuata misingi.


“Ukisoma baadhi ya vifungu vya Katiba, unaweza kuona kuwa Bunge halina mipaka katika kufanya mabadiliko ya Katiba, lakini ukiisoma Katiba yote, utabaini kuwa Bunge lina mipaka na baadhi ya mabadiliko linatakiwa liwaulize wananchi kupitia kura ya maoni,” alisema.


Alisema mara kadhaa Bunge lilipokuwa likiingilia uamuzi wa kimahakama na kuufuta, wao walibaki hawana jinsi, kwa sababu kisheria, Mahakama haiwezi kufungua kesi yenyewe na kuiendesha.


“Mahakama inategemea maoni ya umma. Hukumu ya Mahakama ikifutwa na Bunge, Mahakama yenyewe haiwezi kufungua kesi ili kutoa msimamo wake na kuutetea uhuru wake,” alisema na kuwashauri Watanzania wawe walinzi wa kwanza wa uhuru wa mahakama inapotokea hali kama hiyo.


Bw. Samatta alifafanua akisema kutokana na vitendo hivyo vya Bunge, fursa pekee ya Mahakama ingekuja baada ya wananchi wenyewe kufungua kesi kutaka kuhoji vitendo vya Bunge na kutaka uhuru wa Mahakama uheshimiwe.


“Nakumbuka wakati fulani alikuja mwananchi mmoja kufungua kesi hiyo, akitaka mipaka ya Bunge na Mahakama iwekwe bayana. Niliteua jopo la majaji kusikiliza kesi hiyo, ambayo naamini ingekuwa kubwa na nzito zaidi katika historia ya uhuru wa Mahakama. Mimi mwenyewe nilikuwa katika jopo la majaji tukiwa tayari kuiendesha kesi hiyo.


“Lakini kitu ambacho hadi leo hatujajua sababu yake, ni kwamba yule mwananchi siku ya kuanza kusikilizwa kesi, hakutokea na hata jitihada za kusubiri labda angekuja kutoa udhuru wowote na kuifanya kesi hiyo iendelee, hazikufanikiwa. Tukalazimika kuifuta. Hadi leo hakuna mwananchi mwingine aliyefungua kesi kutaka Mahakama itoe msimamo wake,” alisema.


Akizungumzia suala la uhuru wa Mahakama, hasa kipengele cha bajeti na hoja kuwa mamlaka ya Rais kuteua majaji kama yanaweza kuwa kitanzi katika uhuru wa Mahakama, Bw. Samatta akianzia na suala la bajeti, alisema katika mambo yaliyoikwaza Mahakama katika kipindi alichokuwa mkuu wake ni bajeti.


“Bajeti ya Mahakama ni ndogo sana na katika kipindi chote nilichokuwa katika sekta hiyo, kipindi ambacho tulipewa fedha nyingi basi ni nusu ya kile tulichokuwa tumeomba, mara kadhaa tulipewa hata pungufu ya hapo,” alisema.


Aliongeza: “Bajeti ya Idara ya Mahakama ni ndogo. Nchi nyingine zinatenga bajeti kubwa na zimekuwa na mafanikio. Matatizo mengi ya kushindikana mageuzi katika Mahakama, yanatokana na bajeti kuwa ndogo.”


Alitaja baadhi ya matatizo ambayo bado yanaikumba Mahakama hata baada ya yeye kumaliza muda wake, kuwa ni upungufu wa majengo, vifaa vya kazi, upungufu wa wafanyakazi na pia mishahara midogo.


Alisema iwapo ripoti ya Kamati ya Jaji Bomani itafanyiwa kazi, matatizo mengi yanayoikumba Mahakama ya Tanzania yatatatuliwa.


Akizungumzia suala la kama nguvu alizopewa Rais kuteua majaji akiwamo Jaji Mkuu zinaweza kuathiri uhuru wa Mahakama, alisema suala hilo ni zito na linahitaji mjadala wa umma.


“Labda hilo huko mbele tuliangalie kwa kina. Linahitaji mjadala. Zipo nchi kama India wanatumia mfumo wa Jaji anayefuatia kwa uzoefu ndiye moja kwa moja anakuwa Jaji Mkuu, Rais hateui Jaji Mkuu. Lakini hata hilo linaweza kuwa na matatizo. Hivyo baadaye tunaweza kuruhusu wananchi watafakari faida na hasara za kila mfumo,” alisema.


Katika mahojiano hayo pia Bw. Samatta alisema hakujisikia vibaya wakati akiwa Jaji kumhukumu mtu adhabu ya kunyongwa, kwa sababu wengi waliopewa adhabu hiyo walikuwa wamefanya makosa makubwa na ya kikatili.


“Sikujisikia vibaya kumhukumu mtu kunyongwa, kwa sababu waliopewa, kwanza sheria ya sasa inaruhusu, lakini pia adhabu hiyo hutolewa kwa watu ambao wamefanya makosa makubwa ikiwamo kuua,” alisema na kuzungumzia mwito wa wanaharakati mbalimbali wa haki za binadamu wanaotaka adhabu hiyo sasa ifutwe.


“Naamini nchi yetu itafikia wakati itaruhusu mjadala juu ya hilo. Lakini hata kama ni kuifuta adhabu ya kifo basi hatua hizo zisichukuliwe ghafla.”


Maisha ya ustaafu


Kuhusu maisha baada ya kustaafu, Bw. Samatta, alisema hafikirii kuwa wakili binafsi katika maisha yake ya kustaafu na badala yake atajishughulisha zaidi na kilimo na kujisomea vitabu.


Akizungumza jana katika mahojiano maalumu nyumbani kwake Dar es Salaam, Bw. Samatta alisema haoni kama ni vema kwa mtu kama yeye aliyefikia hadhi ya kuwa Jaji Mkuu, kurejea tena mahakamani na kusimama mbele ya mahakimu au majaji akitetea wateja.


Bw. Samatta alisema hayo alipokuwa akijibu swali la kama anafikiria kufanya kazi za uwakili wa kujitegemea na pia kama alikuwa na mpango wa kuwa mhadhiri wa sheria katika vyuo hapa nchini baada ya kustaafu.


“Sifikirii kuwa wakili wa kujitegemea kwa muda huu. Kuna sababu za kiufundi tu ambazo zinanifanya nione si busara kuifanya kazi hiyo,” alisema na kufafanua:


“Wapo majaji wanapostaafu wamekuwa wakirejea katika kazi za sheria kwa kuwa mawakili binafsi. Lakini kwangu hasa kwa wadhifa nilioufikia, nadhani lipo tatizo la msingi linalonikwaza lakini pia sidhani kama ni busara kurejea mahakamani na kuanza kuwaomba mahakimu na majaji waniruhusu niendeshe kesi kama wakili.”


Akizungumzia mipango yake akiwa mstaafu, Bw. Samatta alisema anapanga kubaki mkulima na zaidi kutumia muda mwingi kusoma vitabu vingi ambavyo anasema alikosa nafasi ya kuvisoma.


“Napanga kubaki mkulima wa kawaida, si kilimo cha biashara, nitalima kama hobby tu,” alisema na kuongeza:


“Nataka kutumia muda wangu mwingi wa mapumziko kusoma vitabu. Nina vitabu vingi sana ambavyo sikupata nafasi ya kuvisoma. Vingi nitakavyosoma sasa ni vilivyo nje ya fani ya sheria. Nina vitabu vingi karibu 100 vya maisha ya watu, siasa na historia ambavyo sijawahi kuvisoma.”


Bw. Samatta pia alisema anafikiria kuandika vitabu, lakini hilo litatokana na kama atapata nyaraka ambazo anajaribu kuzikusanya.


“Nafikiria pia kuandika, lakini kuna nyaraka nazikusanya kwanza nikifanikisha hilo, basi nitaandika kitu ambacho kitakuwa ni mchango wangu katika fani ya sheria na utumishi wangu katika Mahakama,” alisema.


Baada ya kuanza maisha ya ustaafu, Bw. Samatta aliwaomba Watanzania kuiunga mkono Mahakama na kuitumia, kwani ni chombo kilichoundwa kwa ajili ya kusimamia haki zao.


Pia aliomba wananchi wauunge mkono uongozi wa Mahakama ya Tanzania chini ya Jaji Mkuu mpya, Bw. Augustino Ramadhan.


Source: Majira

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents