Sasa zamu ya Mramba, Yona

Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, jana ilipanda joto baada ya mawaziri wa zamani wawili Bw. Basil Mramba na Bw. Daniel Yona, kufikishwa hapo, wakituhumiwa kutumia vibaya madaraka yao wakiwa mawaziri

Mawaziri wa zamani mh. Daniel Yona (shoto) na Mh. Basil Mramba wakiwa katika mahakama ya hakimu mkazi ya kisutu jijini dar baada ya kusomewa mashtaka yao muda mfupi uliopita.

 

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu Dar es Salaam, jana ilipanda joto baada ya mawaziri wa zamani wawili Bw. Basil Mramba na Bw. Daniel Yona, kufikishwa hapo, wakituhumiwa kutumia vibaya madaraka yao wakiwa mawaziri.

Bw. Mramba na Bw. Yona ambao kwa nyakati tofauti waliwahi kuwa mawaziri wa fedha, wanadaiwa kuingia mkataba wenye utata wa uchimbaji madini na kampuni ya M/S Alex Stewart (ASSAYERS) ya Uingereza na tawi lake M/S Alex Stewart (ASSAYERS) Government Business Corporation yenye makao yake Dar es Salaam.

Mawaziri hao walifikishwa mahakamani hapo jana kujibu mashitaka 13 yanayowakabili huku mahakama hiyo ikiwa imefurika wasikilizaji wakiwamo ndugu, jamaa na marafiki wa mawaziri hao.

Akisoma mashitaka dhidi ya mawaziri hao wastaafu, Wakili wa Serikali, Bw. Stanslaus Boniface alidai kuwa kati ya Agosti 2002 na Juni 14, 2004 Dar es Salaam, watuhumiwa wakiwa watumishi wa umma, kwa pamoja walitumia vibaya madaraka kwa kusaini mkataba wenye utata na kampuni hiyo.

Katika mashitaka ya pili, ilidaiwa kuwa Mei 28, 2005 Dar es Salaam, walitumia madaraka yao vibaya na kuiruhusu kampuni hiyo kuendelea kuchimba dhahabu kwa miaka miwili kuanzia Juni 14,2005 hadi Juni 23, mwaka jana kinyume na taratibu za sheria ya manunuzi. Wah. Yonah na Mramba wakiondoka mahakama ya kisutu kuelekea segerea

Wakili huyo aliendelea kudai katika mashitaka ya tatu, kuwa kati ya Machi 2005 na Mei 28, 2005 Dar es Salaam, wakiwa waajiriwa wa Serikali katika wadhifa wa uwaziri, watuhumiwa walitumia vibaya madaraka yao kwa kumwalika Dkt. Enrique Segura wa kampuni ya M/S Alex Stewart (ASSAYERS), kuendelea kufanya kazi kwa miaka miwili bila majadiliano na Serikali.

Bw. Mramba na Bw. Yona katika mashitaka ya nne, wanadaiwa kuwa kati ya Machi 2005 na Mei 28, 2005 Dar es Salaam, waliacha kutembelea mgodi huo na kupatana ada itakayolipwa na kushindwa kuwasilisha makubaliano hayo serikalini na kampuni hiyo kuendelea kufanya kazi kwa miaka miwili kuanzia Juni 14, 2005 baada ya makubaliano kusainiwa Mei 28, 2005 bila suluhu ya ulipaji ada ya kampuni, kwa kuzingatia taratibu stahiki.

Baada ya kusomwa mashitaka hayo manne yaliyowahusu watuhumiwa wote wawili, yaliyosalia yalimhusu Bw. Mramba peke yake, ambapo katika mashitaka ya tano mpaka ya 11, anadaiwa akiwa Waziri, alitumia madaraka yake vibaya kwa kupuuza mapendekezo yaliyotolewa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) ya kutoa msamaha wa kodi kwa kampuni hiyo.

Kwa mujibu wa mashitaka hayo, kati ya Desemba 18 na 19, 2003 alitoa hati namba GN 423/2003 ya msamaha, Desemba 19, 2003 GN 424/2003, Oktoba 15, GN 197/2004 na kati ya Oktoba 14 na 15, 2004 alitoa GN 498/2004.

Anadaiwa pia kuwa Novemba 19, 2005 alitoa GN namba 377/2005 na Novemba 15, 2005 alitoa GN namba 378/2005 ambayo ilitoa msamaha wa kodi yote ya mapato iliyotakiwa kulipwa na kampuni hiyo kinyume na mapendekezo ya TRA.

Katika mashitaka namba 12, Bw. Mramba na Bw. Yona wanadaiwa kuwa kati ya Juni 2003 na Mei 28, 2005 wakiwa mawaziri, kwa makusudi na kwa kudhamiria, walishindwa kuchukua hatua za makusudi za kutekeleza majukumu yao ipasavyo ya kuhakikisha makubaliano yaliyofikiwa na kampuni hiyo ni halali na wakaruhusu msamaha wa kodi na kuisababishia Serikali hasara ya zaidi ya sh. bilioni 13.7.

Ilidaiwa katika mashitaka ya mwisho kuwa kati ya mwaka 2003 na mwaka jana, akiwa Waziri wa Fedha, kwa makusudi Bw. Mramba alishindwa kutimiza wajibu wake akasaini GN 423/2003, 424/2003, 497/2004 na 498/2004, 377/2005 na 373/2005 za msamaha wa kodi kwa kampuni hiyo.

Watuhumiwa hao walikana mashitaka yao wakidai kutohusika na madai hayo wakiwa watumishi wa umma.

Baadaye mawakili wao, Bw. Elias Msuya, Bw. Samweli Mapande, Bw. Mafuru Mafuru, Bw. Joseph Tadeo na Bw. Michael Ngaro wakiongozwa na Bw. Tadeo, waliiomba mahakama kuwapa wateja wao dhamana yenye masharti nafuu kutokana na kwamba walikuwa watumishi wa Serikali na hivyo hawawezi kutoroka.

Hakimu Mkazi wa Mahakama ya hiyo, Bw. Hezron Mwankenja, alisema kutokana na ombi la mawakili hao kuwa la msingi, aliiweka dhamana wazi kwa watuhumiwa hao kwa masharti manne, likiwamo la kulipa fedha taslimu sh. bilioni 3.9 kila mmoja.

Pia pasipoti zao za kusafiria zihifadhiwe na Mahakama na kila mshitakiwa asitoke nje ya Dar es Salaam na kuwa na wadhamini wawili wawili ambao watathibitishwa na Mahakama.

Washitakiwa hao walifikishwa mahakamani hapo na Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) baada ya kukamilisha uchunguzi wao uliochukua takriban miaka mitatu.

Hata hivyo, jana walishindwa kutimiza masharti ya kutoa fedha taslimu sh. bilioni 3.9 wakarudishwa rumande.

Kesi hiyo iliahirishwa hadi Desemba 2 mwaka huu, itakapotajwa na endapo watuhumiwa watatimiza masharti hayo, watakuwa nje kwa dhamana mpaka kesi yao itakapotajwa.

Source: Eben-Ezery Mende na Hilary Komba – Majira

 

 

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents