Siasa

Seif anitambue Kama Mimi ndio Raisi ndio tujadili Muafaka

Raisi wa Zanzibar Amani Abeid KarumeRaisi wa Zanzibar Amani Abeid Karume, ametoa masharti ya kukutana na Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, kuhusu Muafaka na kumtaka kwanza amtambue kuwa ni Rais halali aliyechaguliwa kwa kura nyingi

Raisi wa Zanzibar Amani Abeid Karume, ametoa masharti ya kukutana na Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad, kuhusu Muafaka na kumtaka kwanza amtambue kuwa ni Rais halali aliyechaguliwa kwa kura nyingi kwenye uchaguzi mkuu mwaka 2005.

 

Akizungumza jana na waandishi wa habari Ikulu visiwani hapa baada ya kurudi safari ya Marekani, Rais Karume alisema kimsingi hana matatizo na Maalim Seif kukutana naye na kuzungumzia mustakabili wa kisiasa nchini, lakini amtambue kwanza kuwa ni Rais aliyechaguliwa kwa kura nyingi kuongoza visiwa vya Unguja na Pemba.

 

“Milango iko wazi kwa mtu yeyote kukutana nami…hata ninyi waandishi wa habari si mnakuja hapa…lakini masharti ni lazima anitambue mimi kama Rais halali niliyechaguliwa kwa kura nyingi katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2005,” alisema Rais Karume.

 

Alisema hilo kutokana na swali aliloulizwa kuhusu moja ya masharti ambayo CUF inayatoa kwa sasa ili kuanza tena kwa mazungumo ya Muafaka wa kisiasa, kati ya vyama hivyo ambao kwa sasa unaonekana wazi kukwama.

 

CUF wanataka ili kurudi katika meza ya mazungumzo ya Muafaka, Rais Jakaya Kikwete kwanza aingilie kati na kuwakutanisha Maalim Seif na Rais Karume, hatua ambayo itawezesha mazungumzo hayo kuanza tena baada ya kukwama.

 

Mazungumzo ya Muafaka kati ya CUF na CCM kwa sasa yamekwama na juhudi zinafanywa ili viongozi wa pande mbili hizo, warudi kwenye mazungumzo katika hatua za mwisho ili Muafaka huo upate kufanya kazi.

 

Rais Karume alisikitishwa na kauli ya CUF ya kupinga kura ya maoni katika suala zima la Muafaka ambapo ni moja ya uamuzi uliofikiwa na Halmashauri Kuu ya CCM kijijini Butiama, Musoma, Mara.

 

Alisema kura ya maoni ndio utaratibu mzuri unaokubalika katika kutoa na kusikiliza matatizo ya wananchi kuhusu jambo fulani na kuongeza kwamba si vizuri watu wawili kuwaamuliwa wengi katika jambo kubwa lenye maslahi kwa Taifa.

 

“Watu kuulizwa ndio utaratibu unaokubalika duniani kote katika nchi yenye kufuata demokrasia na utawala bora…nawashangaa sana hawa CUF ambao wanajidai kwamba wana nguvu ya umma,” alisema Rais Karume na kuongeza kuwa uamuzi wa watu wawili katika jambo la maslahi ya Taifa ni dhima kubwa na ni sawa na udikteta,” alisema Rais.
“Nashindwa kuelewa hawa CUF wanachoogopa ni nini kwa sasa, hasa katika suala la kuhakikisha unapatikana Muafaka…watu kuulizwa katika suala la Muafaka na mwelekeo wa Serikali ya visiwa vya Unguja na Pemba ni lazima, ambapo kisanduku kitatumika katika kupata maoni ya hatma za siasa za visiwani Zanzibar.

 

Mpaka kufikia hivi sasa Chama cha CUF kinapinga kuhusu mwelekeo wa kuwapo kwa kura ya maoni, kwa sababu mbalimbali ikiwamo kuhofia kuwapo kwa udanganyifu na kuibiwa kura katika suala hilo, wakichukulia uchaguzi mara tatu katika mfumo wa siasa za vyama vingi kura zao ziliibuliwa na CCM.

 

Rais Karume alisema kuwa kura ya maoni kuhusu mustakabali wa siasa za visiwa vya Unguja na Pemba zitapigwa na Wazanzibari wenyewe na hakuna mtu kutoka sehemu nyingine ambaye atapiga kura hiyo.

 

Hata hivyo Rais Karume aliongeza kuwa si sera ya CCM kubagua Wapemba kama inavyodaiwa, lakini yeye amechaguliwa kwa kura nyingi na wafuasi wa CCM ambao wanatoka Unguja, hivyo kwa mujibu wa mfumo uliopo sasa, anatakiwa kuunda Baraza la Mawaziri kwa kutumia wajumbe waliomchagua.

 

“Mimi nimepata kura 20,000 tu katika kisiwa cha Pemba…nimechaguliwa kwa kura nyingi ambazo nimepigiwa na watu wa Unguja sasa hawa CUF wanachokilalamikia ni kipi…hapa tunafuata mfumo wa Uingereza, anayepata kura nyingi anaunda Serikali,” alisema Rais Karume.

 

Aidha aliitaka CUF kuacha chokochoko na maneno ambayo mwelekeo wake ni kuwabagua wananchi wa visiwa hivi sambamba na kupuuza kuwepo kwa vikaratasi vinavyosambazwa vikiwataka wananchi wa Pemba kuondoka Unguja na kusema ni upuuzi mtupu.

 

Alisema fitna hizo zinazofanywa na baadhi ya watu wachache ambao hawawatakii mema wananchi wa Unguja na Pemba, zinahatarisha amani na utulivu uliopo sasa na kuvitaka vyombo vya habari kulifanyia kazi suala hilo.

 

“Nyie waandishi wa habari acheni kuandika habari za uchochezi na kugombanisha wananchi…nyie hamna kinga mnaweza kufikishwa mahakamani….mimi nawachukia sana waandishi wa habari wa aina hiyo,” alisema Rais Karume.

 

 

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents