Technology

Sekta ya mawasiliano ya simu inavyokua kwa kasi nchini Tanzania

Mwaka mpya ni wakati wa kutafakari yaliyopita, tulipokosea, tulipofanikiwa na namna gani tufanye vizuri zaidi. Tumeingia pia muongo mpya (2020 hadi 2030) kwa hiyo pia ni miaka kumi kutafakari nini tumefanya miaka 10 iliyopita na nini tufanye miaka 10 ijayo.

Bila shaka muongo uliopita (2010 hadi mwisho wa 2019) umeleta mabadiliko mengi sana. Moja ya mabadiliko makubwa ya muongo huu tunaoumaliza ni maendeleo ya teknolojia hasa katika mawasiliano ya simu za mkononi.

Simu sasa imekuwa sehemu ya maisha, takwimu za siku za karibuni zikionyesha kuwa kuna watumiaji wa simu zaidi ya milioni 25 nchini (si watumiaji wa laini za simu, hao ni wengi zaidi kwa sababu simu moja yaweza kuwa na laini zaidi ya moja).Lakini unafahamu kwamba mwaka 2010 idadi hiyo ilikuwa chini ya milioni 15? Wataalamu wanasema kwamba kufikia mwaka 2025 idadi hiyo itazidi watu milioni 35, na kufikia karibu asilimia 50 Watanzania.

Pengine moja ya maeneo ambayo maendeleo ya sekta ya mawasiliano ya simu yanaonekana wazi zaidi ni katika kuenea kwa kasi kwa mtandao wa intaneti. Takwimu zinaonyesha kwamba katika muongo mmoja uliopita idadi ya watumiaji wa intaneti nchini imeongezeka maradufu.

Hebu fikiria, mwaka 2010 ni asimilia 5 tu ya Watanzania walikuwa wanapata huduma ya mtandao wa intaneti kwa njia ya simu na kati yao ni asilimia 5 tu walikuwa maeneo ambayo wangekuwa kupata 3G (wakati huo ndiyo ilikuwa kasi kubwa zaidi).

Miaka 10 baadaye, hii leo zaidi ya asilimia 60 ya nchi inaishi katika mikoa yenye 3G na kwa wastani mtu mmoja kati ya kila watu wa nne ana huduma ya intaneti kupitia simu yake ya mkononi.

Haya ni maendeleo makubwa sana lakini hata hivyo tusiyachukulie kuwa ni kazi rahisi kwani ni matokeo ya uwekezaji wa kimkakati katika muongo mzima na hii imewezekana tu kwa kuwa na mazingira bora ya uwekezaji. Yako mambo mengi ambayo huyapa afya mazingira ya uwekezaji katika sekta ya mawasiliano ya simu na mojawapo ni idadi ya makampuni katika soko.

Inaelezwa kwamba soko lenye kampuni chache zenye kufanya shughuli zake kwa pamoja (market consolidation) ni jambo mojawapo linaloleta mazingira yenye afya ya kiuwekezaji kwenye sekta hii.

Mwaka 2019 soko la mawasiliano nchini limeanza kuelekea huko kwa idadi ya kampuni kupungua. Oktoba 2019 kampuni ya Smart ilifunga kazi zake na kuondoka sokoni na mwezi mmoja baadaye (Novemba 201) Tigo na Zantel wakaunganisha shughuli zao.

Hii inapanua uwekezaji makini zaidi na mkubwa wenye tija kwa wateja na uchumi kwa ujumla. Hatua njema lakini kazi zaidi inahitajika katika kuendelea kujenga mazingira rafiki zaidi kukuza uwekezaji wa kampuni hizi na kutupa huduma bora zaidi. 2019 ilikuwa njema kwa sekta hii, tutarajie 2020 njema zaidi.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents