Technology

Sekta ya mawasiliano ya simu nchini ina mafanikio makubwa lakini tusibweteke tuboreshe zaidi

Msimu wa shamrashamra za sikuku za mwisho wa mwaka umefika ukingoni na sote tunaishukuru sana teknolojia ya mawasiliano ambayo hakika imechangia kusaidia mawasiliano yetu na wale tuwapendao, katika msimu huu. Hata wale ambao walishindwa kusafiri kujiunga na wapendwa wao msimu huu walau waliweza kuzungumza nao au hata kuwapigia video call.

Sekta ya mawasiliano ya simu kwa hakika imebadili maisha yetu. Katika Afrika, eneo la Kusini mwa Jangwa la Sahara, sekta ya mawasiliano ya simu za mkononi nchini Tanzania imekuwa ni ya kupigiwa mfano hasa kwa namna ambavyo watumiaji simu wanavyoongezeka siku hadi siku na jinsi mtandao wa intaneti unavyosambaa maeneo mbalimbali nchini.

Licha ya mafanikio hayo, daima tunaweza kuboresha zaidi.
Tanzania ni moja ya nchi zenye makampuni mengi zaidi ya simu barani Afrika. Hili laweza kuonekana kama jambo zuri lakini hata hivyo wataalamu wa masoko ya mawasiliano na uwekezaji katika sekta hiyo wanaeleza kuwa masoko mengi bora ya mawasiliano ya simu duniani ni yale ambayo yana kampuni chache zenye uwekezaji imara. Katika masoko ya aina hiyo wateja na nchi wanapata tija zaidi. Wanaendelea kueleza kuwa kama kampuni hizo zingeunganisha nguvu katika shughuli zao ingeongeza faida na uwekezaji wenye tija zaidi kwa wateja katika eneo la bei ya huduma na ubora.

Bahati nzuri hili limeanza kufanyika kwa kiasi fulani. Oktoba 2019 kampuni ya Smart ilijiondoa soko la Tanzania na kuacha makampuni 6 sokoni. Mwezi Novemba mwaka 2019 kampuni mbili kubwa za Tigo na Zantel nazo zikaunganisha shughuli zao na kufanya jumla ya makampuni sokoni sasa kuwa 5. Kama wataalamu wanavyoeleza, hii inamaanisha ni jambo jema japo kuna nafasi ya kuendelea kupunguza namba ya wachezaji na kuongeza ubora na tija zaidi kwa nchi na wateja kuanzia bei za vifurushi hadi ubora na upatikanaji wa mtandao. Mwaka ndio umeanza sasa, tutumaini kuwa kutakuwa na maboresho zaidi katika sekta hii ambayo yataleta tija si tu kwa serikali kwenye kodi lakini pia kwetu watumiaji wa simu ili tuendelee kufurahia mapinduzi haya ya kiteknolojia na mawasiliano.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents