Serikali ina matumizi makubwa mno – CAG

Licha ya mapato ya taifa yanayokusanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuongezeka katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, serikali inakabiliwa na tatizo la matumizi makubwa,

Na Joseph Mwendapole, Dodoma



 


Licha ya mapato ya taifa yanayokusanywa na Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kuongezeka katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, serikali inakabiliwa na tatizo la matumizi makubwa, taarifa ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Bw. Ludovick Utouh, imesema.

Mkaguzi huyo amezidi kufahamisha katika ripoti ya serikali ya mapato na matumizi ya fedha kwa mwaka wa fedha ulioishia Juni 30, 2007, iliyotolewa hivi karibuni kwamba mwaka wa fedha ulioishia Juni 30, 2007, TRA ilikusanya Sh. bilioni 254 ikiwa ni zaidi ya malengo iliyojiwekea ya kukusanya sh. bilioni 241.

Hata hivyo, Bw. Utouh alisema mfumo wa matumizi ya mapato kwa serikali umekuwa ukiongezeka mara dufu kuliko kiasi cha kinachokusanywa.

Alibainisha kuwa matumizi makubwa yanaweza kusababishwa na ukosefu wa viwango vya magari na samani ambazo serikali inanunua pamoja na kushindwa kudhibiti matumizi ya fedha katika kukarabati magari na matumizi mabaya ya mafuta.

Alitaja eneo lingine ambalo linachangia matumizi makubwa serikalini ni maofisa wake kufanya utitiri wa semina na warsha ndani na nje ya nchi.

Aidha alisema katika ukaguzi huo, imebainika kwamba serikali ni dhaifu katika kudhibiti manunuzi ya samani kwa maofisa wake.

Alisema kwa mfano, mara nyingi samani zinazowekwa katika nyumba za serikali zimekuwa zikinunuliwa kutegemeana na matakwa ya ofisa au mtumiaji, hali inayochangiwa na kutokuwa na viwango vya pamoja ambavyo serikali imejiwekea.

Alishauri kuwa moja ya mambo yanayoweza kupunguza matumizi makubwa ya fedha ni kwa serikali kuwa na viwango vya aina ya magari na samani inayozihitaji kwa taasisi zake na kudhibiti matumizi makubwa ya mafuta.

Katika hatua nyingine, Bw. Utouh alisema misamaha ya kodi isiyo ya lazima imechangia TRA kushindwa kukusanya kodi mara dufu.

Alisema licha ya TRA kukusanya zaidi ya Sh. bilioni254 kwa mwaka 2006/07, mamlaka hiyo ingeweza kukusanya zaidi ya hapo iwapo misamaha ya kodi isiyo ya lazima isingetolewa.

Alisema katika kipindi hicho, misamaha ya kodi ya asilimia 30 ilitolewa, hali ambayo iliifanya TRA isiweze kukusanya zaidi. Kufuatia hali hiyo, Bw. Utouh aliishauri serikali kupitia upya sera yake ya kutoa misamaha ya kodi kwa lengo la kuipunguza.

“Mapendekezo makubwa katika ukusanyaji wa kodi, serikali ipitie upya sera yake ya kutoa misamaha iliipunguzwe hadi kufikia kiasi ambacho inaweza kuvumilika na itolewe kwa kuzingatia maslahi ya umma,“ alishauri.


 


Source: Nipashe

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents