Habari

Serikali ya Tanzania yatangaza kuuza Mamba na Viboko, Waziri Kigwangalla aeleza sababu

Waziri wa Maliasili na Utalii, Dkt. Hamis Kigwangalla amesema Serikali ya Tanzania itaanza kuuza 10% ya Mamba wote nchini pamoja na kupiga mnada Viboko kwa kile alichokieleza kuwa kumekuwa na ongezeko kubwa la wanyama wakali kuingia katika makazi ya watu.

Dkt.  Kigwangalla amesema hayo kupitia kurasa zake za mitandao ya kijamii na kusema kuwa wataweka uzio katika maeneo yote ambayo wanyama hao walishawahi kuua watu ili iwe kumbu kumbu.

Tumeamua kuuza asilimia 10 ya mamba wote nchini! Pamoja na kuamua kuuza asilimia 10 ya mamba wote nchini, pia tunaanzisha mradi wa kuweka uzio kwenye maeneo yenye historia ya matukio ya mamba kudhuru watu, kama Maleza na Ruvu. Tunawaomba wananchi wasifanye mauaji ya kulipiza kisasi tukitekeleza haya, pia waache tabia hatarishi! Sambamba na maamuzi haya, tunaanzisha vituo vya kudumu vya ulinzi kwenye maeneo yote korofi, ambapo wanyama wakali/waharibifu kama Tembo na Simba wamekuwa wakileta shida kwa wananchi. Tutaendelea pia kufundisha wananchi namna ya kujisalimisha kama wakikutana na wanyamapori. Aidha, tutauza viboko wote waliopo kwenye maeneo yenye maji kama maziwa, mabwawa na mito iliyopo mjini, kama vile pale Mpanda, Mafia na Babati. Mauzo ya wanyama hawa yatafanyika kwa njia ya mnada kwa utaratibu ambao utatangazwa wiki ijayo. Maamuzi ya kupiga mnada maliasili hizi ili kupunguza migogoro kati ya wanadamu na wanyamapori yamekuja baada ya kukamilika kwa utafiti nilioagiza ufanywe na TAWIRI (Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania) mnamo Julai 2018 nilipofanya ziara ya #PoriKwaPori nikiwa Ziwa Rukwa. Ninawashukuru wabunge wenzangu wote kwa uelewa, na zaidi kwa kulipa kipaumbele jambo hili la migogoro baina ya wanadamu na wanyamapori, waathirika zaidi wakiwa Mhe. Mulugo, Mhe. Dau, Mhe. Hamoud, Mhe. Bwanausi, Mhe. Getere na Mhe. Njalu. Ushauri wenu umetusaidia kufikia hapa.” Ameeleza Kigwangalla.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents