Habari

Serikali kuendelea kuratibu juhudi za kukuza ajira nchini

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Serikali imeendelea kuratibu juhudi za kukuza ajira nchini hadi kufikia mwezi Februari mwaka huu, jumla ya ajira 482,601 katika sekta rasmi zimezalishwa nchini.

Waziri Mkuu ameyasema hayo leo, wakati akitoa hotuba kuhusu mapitio ya mwelekeo wa kazi za serikali na makadirio ya mapato na matumizi ya fedha za ofisi ya Waziri Mkuu na ofisi ya Bunge kwa mwaka 2018/2019.

“Mheshimiwa Spika, katika mwaka 2017/2018, Serikali imeendelea kuratibu juhudi za kukuza ajira nchini. Hadi kufikia mwezi Februari 2018, Jumla ya ajira 482,601 katika sekta rasmi zimezalishwa nchini. Kati ya ajira hizo ajira 345,547, sawa na asilimia 72 zimezalishwa kutokana na shughuli za umma ikiwemo miradi ya maendeleo ya Serikali kama vile ujenzi wa reli ya kisasa (SGR), ujenzi wa miundombinu ya barabara, maji na miradi ya TASAF na ajira 137,054 sawa na asilimia 28 zimezalishwa katika sekta binafsi,” amesema Waziri Mkuu.

“Mheshimiwa Spika, Serikali inaandaa mpango mkakati wa kuhakikisha kwamba Watanzania wazawa wanashiriki na kunufaika na miradi mikubwa ya kitaifa. Vikao kati ya Serikali na wafanyabiashara vimefanyika ili kuwaandaa kuwa sehemu ya utekelezaji wa mkakati huo. Katika mwaka 2018/2019, Serikali itaendelea kuratibu masuala ya ukuzaji ajira nchini ikiwa ni pamoja na kukamilisha mapitio ya Sera ya Taifa ya Ajira ili iendane na mahitaji ya sasa ya soko la ajira,” aliongeza Waziri Mkuu.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents