Habari

Serikali kuendelea kutoa dawa za kutibu sumu ya nyoka

Serikali imesema itaendelea kutoa dawa zinazotibu sumu ya nyoka ili kupambana na tatizo hilo nchini.

Kauli hiyo ya serikali ilitolewa Dar es Salaam jana na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu.

“Kama tunavyofahamu nchi yetu ina aina mbalimbali za nyoka ambao pindi wakimuuma mtu huleta madhara mbalimbali ya kiafya. Aidha tunafahamu kwamba tatizo hili lipo zaidi katika maeneo ya vijijini ambako uwezo wa wananchi kumudu gharama za matibabu ni mdogo.”

Alisema dawa za kutibu sumu ya nyoka huagizwa kutoka nje ya nchi; na kwamba si tu hazipatikani kwa urahisi, bali pia zinapatikana kwa gharama kubwa. Waziri huyo alisema bei ya kununulia dawa hizo ni kati ya dola za Marekani 55 hadi 85 (yaani Sh 118,250 hadi 182,750) kwa kichupa kidogo kimoja.

Alisema kichupa hicho huweza kutumika kwa wagonjwa wanne, lakini mara tu baada ya kufunguliwa dawa hiyo huwa haifai tena kutumika ndani ya mwezi mmoja tu.

Waziri alisema pamoja na changamoto hizo, Serikali kupitia Bohari Kuu ya Dawa (MSD) kila mwaka huagiza dawa hizo kwa ajili ya mahitaji hayo ya kutibu wagonjwa walioumwa na nyoka, ambapo bei ya kuinunua kutoka MSD ni shilingi 200,000 kwa kichupa kimoja.

“Hospitali zetu mbalimbali zimekuwa zikiagiza dawa hizi kutoka MSD na kwa wasambazaji wengine kwa bei hii au zaidi na kuwatibu waathirika wanaohitaji dawa za sumu za nyoka mara zinapohitajika. “Napenda kuwakumbusha kwamba kwa mujibu wa Sera ya Afya ya mwaka 2007, huduma za tiba hutolewa bure kwa makundi maalumu au kwa kuchangiwa kwa sehemu ya gharama, au kwa kupitia mfumo wa bima mbalimbali za afya kama vile CHF.

“Kwa wale wasio na uwezo na wanaothibitishwa kuwa hawana uwezo, utaratibu wa msamaha hutumika,” alisema Waziri.

Alisema katika kuhakikisha kwamba wananchi wanaohitaji dawa ya sumu ya nyoka wanahudumiwa ipasavyo, waganga wakuu wa mikoa na viongozi wa hospitali zote nchini, wanatakiwa kuhakikisha hospitali zote za umma zinaingiza dawa hiyo katika dawa za dharura ili iweze kununuliwa kama dawa zingine za dharura kupitia kifungu cha fedha za dawa za dharura.

Alisema kwa wagonjwa ambao watakuwa na bima ya afya, gharama za matibabu hayo zitalipwa kwa kupitia utaratibu huo wa bima.

“Wananchi wanahimizwa kujiunga na Bima za Afya (CHF/ NHIF) ili kupata unafuu wa matibabu haya na mengine. Mfano CHF gharama ya kujiunga katika halmashauri mbalimbali kwa kaya ni kati ya shilingi 5,000 hadi shilingi 30,000 kwa mwaka.

“Kwa wagonjwa ambao watakuwa hawana bima ya afya, watatakiwa kuchangia gharama hiyo kwa nusu ya bei ya gharama ya dawa hizi au kwa kiwango kingine kitakachoamuliwa na Mganga Mkuu wa Serikali kadri itakavyohitajika.

“Hii ni kutokana na ukweli kwamba kung’atwa na nyoka ni ajali na wananchi wengi wanaopatwa na ajali hii wapo maeneo ya vijijini ambao kimsingi uwezo wao wa kumudu gharama hizi kubwa za matibabu ya dawa ya sumu ya nyoka ni mdogo,” alisema Waziri Ummy.

Alisema wagonjwa watakaothibitika kuwa hawana fedha za kuchangia gharama hiyo, hospitali husika kwa kupitia mpango wa msamaha wa kulipia huduma za afya, wahakikishe kwamba wanampatia mgonjwa huduma hizo kwa utaratibu wa msamaha wa gharama hizo.

BY: EMMY MWAIPOPO

CHANZO: HABARILEO

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents