Siasa

Serikali kumuenzi Amina Chifupa

Serikali imesema itamuenzi marehemu Amina Chifupa kwa kuongeza mapambano dhidi ya dawa za kulevya.

Na Emmanuel Lengwa



Serikali imesema itamuenzi marehemu Amina Chifupa kwa kuongeza mapambano dhidi ya dawa za kulevya.


Kauli hiyo ilitolewa jana na Waziri wa Usalama wa Raia, Bw. Bakari Mwapachu aliyemwakilisha Rais Jakaya Kikwete wakati wa kutoa heshima za mwisho kwa mwili wa marehemu Amina, nyumbani kwake, Mikocheni, jijini Dar es Salaam.


Waziri Mwapachu alisema kifo cha Mbunge huyo kijana, ni pigo kwa taifa kutokana na ujasiri na msimamo wake katika vita dhidi ya dawa za kulevya.


`Amina Chifupa alikuwa jasiri aliyejitolea kushirikiana na wizara yangu katika kupambana na biashara haramu ya dawa za kulevya, tutahakikisha tunamuenzi kwa kuongeza mapambano dhidi ya biashara hiyo haramu,` alisema Waziri Mwapachu.


Aliwataka vijana wote nchini kumuenzi marehemu Amina kwa kuachana na biashara hiyo pamoja na utumiaji wa dawa za kulevya.


`Njia pekee ya kumuenzi ni kwa vijana kujiepusha na matumizi na biashara hiyo kwa vitendo, pamoja na kuacha maovu yote,` alisema.


Pia Waziri Mwapachu alitoa ubani wa Shilingi milioni moja kwa niaba ya Serikali.


Naye Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, Bw. Sitta alisema taifa limempoteza kijana chipukizi na jasiri mwenye upeo mkubwa wa kujenga hoja za kutetea haki.


`Amina alikuwa kijana aliyechipua na kuonyesha kuwa tegemeo la taifa, uwezo wake wa kujenga hoja, ujasiri na ucheshi wake, utakumbukwa daima na Bunge, ni wazi kuwa taifa limempoteza kijana shupavu,` alisema Spika Sitta.


Souce: Nipashe

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents