Habari

Serikali `kuwashukia` vichwangumu wa mifuko…

Serikali imeagiza kampuni zote zinazotengeneza mifuko laini ya plastiki kusitisha mara moja uzalishaji wa mifuko hiyo.

Na John Ngunge, Dodoma



Serikali imeagiza kampuni zote zinazotengeneza mifuko laini ya plastiki kusitisha mara moja uzalishaji wa mifuko hiyo.


Agizo hilo lilitolewa bungeni jana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano), Dk. Hussein Ali Mwinyi, wakati akiwasilisha hotuba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, kuhusu makadirio ya matumizi ya Ofisi hiyo kwa mwaka wa fedha 2007/2008.


Alisema baadhi ya kampuni hapa nchini zinaendelea kukaidi agizo la serikali la kupiga marufuku utengenezaji wa mifuko laini ya plastiki.


Bila kutaja majina, Dk. Mwinyi alitaka kampuni hizo kusitisha uzalishaji wa bidhaa hiyo mara moja.


Alisema, katika utekelezaji wa agizo la serikali, baadhi ya halmashauri za wilaya, miji, manispaa, na jiji, ilibainika kuwa mifuko laini bado inatengenezwa nchini na baadhi ya kampuni.


Waziri alisema, Ofisi ya Makamu wa Rais kwa kushirikiana na Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC), iliendelea kuratibu utekelezaji wa tamko la serikali la kupiga marufuku utengenezaji, uagizaji, uuzaji, ununuzi na matumizi ya mifuko ya plastiki laini na ile ya kufungia maji na maji ya matunda.


Alisema ofisi hiyo kwa kushirikiana na Wizara ya Katiba na Sheria, iliandaa kanuni za kutekeleza tamko hilo, kanuni ambazo zilianza kutumika Oktoba Mosi, mwaka jana.


Aidha alisema, NEMC lilifanya ukaguzi wa kushitukiza kwa baadhi ya viwanda na maduka makubwa yaliyopo Dar es Salaam na kubaini utekelezaji wa agizo hilo ulisababisha baadhi ya wafanyakazi kupoteza kazi na viwanda kupoteza mapato.


Hata hivyo, alisema agizo hilo limezaa matunda mazuri kwa kupungua kwa taka za plastiki katika mazingira.


Kwa mujibu wa Dk. Mwinyi, NEMC inaendelea kushirikiana na wenye viwanda kutafuta mifuko mbadala.


Akizungumzia kuhusu suala la utafutaji na uchimbaji wa mafuta na gesi kuwa la muungano au la, Dk. Mwinyi alisema, serikali zote mbili za Muungano na ya Mapinduzi Zanzibar, zinatambua umuhimu wa nishati hiyo kwa maendeleo ya taifa na zilikubaliana kuwa kabla ya kufanya maamuzi mengine ni vema atafutwe mshauri mwelekezi ili aweze kushauri namna bora ya kushughulikia suala hilo.


Alisema kwa sasa Wizara ya Nishati na Madini kwa kushirikiana na Shirika la Maendeleo la Mafuta (TPDC), zimeandaa rasimu ya hadidu za rejea ambazo zitatumiwa na mshauri mwelekezi katika kufanya kazi hiyo.


Source: Nipashe

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents