Serikali: Watanzania Afrika Kusini wako salama

SERIKALI imesema Watanzania wote waishio Afrika Kusini wako salama kufuatia vurugu zilizozuka nchini humo zilizotokana na wenyeji kuwashambulia na kuwaua wageni kutoka nchi zingine

Na Joyce Magoti

 

SERIKALI imesema Watanzania wote waishio Afrika Kusini wako salama kufuatia vurugu zilizozuka nchini humo zilizotokana na wenyeji kuwashambulia na kuwaua wageni kutoka nchi zingine.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bw. Bernard Membe aliwaambia waandishi wa habari Dar es Salaam jana kuwa Watanzani 98 walikimbilia kituo cha Polisi cha Kati mjini Johannesburg na kwamba watatu kati yao, walipata majera madogo kutokana na misukosuko ya kukimbia kwa ajili ya kutafuta hifadhi.

Bw. Bernard Membe alisema uchambuzi uliofanywa umebaini kuwa Watanzania 77 kati ya hao 98 waliohifadhiwa katika kituo hicho hawana hati za uraia wa Tanzania wala pasipoti za kusafiria.

“Uchambuzi uliofanywa umebaini kuwa Watanzania 21 tu ndio wenye hati halali ya uraia na pasipoti za kusafiria kwenda nchini humo, wengine 77 hawana pasipoti wala hati halali ya kuishi nchini humo licha ya wao kuozungumza lugha ya Kiswahili kwa ufasaha,” alisema Bw. Membe.

Bw. Membe alisema hivi sasa jitihada zinafanyika kwa kushirikiana na viongozi wa Afrika Kusini kuwahoji hao watu hao 77 ili kubaini utaifa wao.

“Hatutashangaa kama kweli hao watakuwa ni wenzetu au ni kutoka katika mataifa mengine kwani kuna nchi nyingi zinatumia lugha ya Kiswahili ili tusije tukabeba mzigo wa wengine,” alisema Bw. Membe.

Alisema lengo la kuwahoji Watanzania hao ambao hawana hati halali ya uraia wa Tanzania ni kujaribu kuepuka kubeba mzigo wa wengine endapo vurugu hizo zitaendelea kwa kulazimika kuwasafirisha na kuwarejesha nchini.

“Watu hao wamedai kuwa ni Watanzania ambapo walizamia katika nchi hiyo kwa ajili ya kutafuta maisha, lengo letu kuwahoji ni zuri kwani vurugu hizo zikiendelea tutalazimika kuwarejesha nchini,” alisema.

Aliongeza kuwa kufuatia vurugu hizo Tanzania itaishawishi Jumuiya ya Kimataifa kulaani vitendo hivyo ili nchi hiyo iache tabia ya kufukuza wageni wanapoingia nchini mwao kwani tabia ya waafrika ni ukarimu na uzalendo.

Vurugu hizo zilizuka hivi karibuni nchini Afrika Kusini baada ya wenyeji kuanza kuwapiga na kuwafukuza wageni waishio nchini humo na kusababisha vifo vya watu zaidi ya 24 na mamia kukimbilia kanisani na misikitini kuomba hifadhi.

 

 

 

Source: Majira

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents