Habari

Serikali yaagiza ufuta kuuzwa kwa mfumo wa stakabadhi

Waziri Mkuu, Kassim Majawaliwa amesema serikali imemuagiza Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi, Dkt. Charles Tizeba kukutane na bodi ya mazao mchanganyiko kwa ajili ya kuliondoa zao la ufuta na kuliingiza katika mfumo wa stakabadhi ghalani.

Waziri Mkuu ametoa kauli hiyo Jumatatu hii, wakati akisalimiana na wananchi katika vijiji vya Nangano, Kibutuka na Kiangara alipowasili katika wilaya ya Liwale kwa ajili ya ziara ya kikazi mkoani Lindi.

Kauli hiyo imekuja baada ya mbunge wa jimbo la Liwale, Mheshimiwa Kuchauka pamoja na wananchi kuiomba Serikali iwasaidie kuboresha bei ya zao la ufuta ambayo imekuwa ikiyumba.

“Tatizo lipo kwenye mfumo wa uuzaji zao la ufuta, unauzwa kwa bei ya rejareja, wanunuzi wako huru. Serikali imemuagiza Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi kuliondoa zao katika bodi ya mazao mchanganyiko na kuliingiza katika mfumo wa stakabadhi ghalani ili kuboresha bei yake,” alisema Waziri Mkuu.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu amemwelekeza Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Liwale Bw. Justine Monko kuhakikisha anamaliza tatizo la maji katika vijiji vya Nangano,Kibutuka na Kiangara.

Na Emmy Mwaipopo

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents