HabariUncategorized

Serikali yaanza kujenga mitambo kuimarisha usikivu wa redio ya taifa

Serikali imeanza kutekeleza Mpango wa kujenga mitambo ya FM nchini kuimarisha usikivu maeneo mbalimbali ili wananchi waweze kupata matangazo kutoka redio yao ya Taifa (TBC).

Kauli hiyo imetolewa leo Bungeni mjini Dodoma na Naibu Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Anastazia Wambura alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Kyerwa Innocent Sebba Bilakwate kwa niaba ya Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe, lililohoji ni lini Serikali itawapatia Wananchi wa Kyerwa haki yao ya kusikiliza Redio TBC ili kujua yanayoendelea katika nchi yao kama ilivyokuwa hapo awali kabla ya kubadilisha teknolojia ya habari badala ya sasa kusikiliza Redio Rwanda na Uganda.

Mpango huo unatekelezwa na Serikali kupitia Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) ambao umeanza kutekelezwa katika wilaya za Kibondo, Nyasa, Longido, Tarime pamoja na Rombo na utaendelea katika wilaya nyingine ikiwemo Kyerwa kadiri bajeti inavyoendelea kuimarika.

“Kwa sasa kama ilivyobainishwa katika Hotuba ya Bajeti ya Wizara ya mwaka 2017/2018, Serikali inaendelea kubadilisha mfumo wa urushaji matangazo kupitia satelaiti uweze kuwa wa kisasa ili kuboresha usikivu wa radio ya Taifa TBC hatua itakayosaidia wananchi kuendelea kupata habari kupitia viongozi wao” amesema Naibu Waziri Wambura.

Naibu Waziri Wambura amebainisha kuwa zipo wilaya 84 nchini ambazo usikivu wa TBC umeshuka na kusababisha baadhi ya maeneo kukosa matangazo ya redio kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo uchakavu wa baadhi ya miundombinu ya radio, uwepo wa milima na uharibifu wa vifaa kutokana na radi wakati wa mvua.

Aidha, Naibu Waziri Wambura amewataka Wabunge na wananchi kuendelea kushirikiana na Serikali kwa kutoa taarifa endapo kutatokea uharibifu wa vifaa vya kusaidia upatikanaji na usikivu wa matangazo ya radio ya taifa TBC katika maeneo yao ili yaweze kufanyiwa marekebisho mapema na wananchi waendelee kupata habari mbalimbali za Kitaifa na Kimataifa.

Wilaya ya Kyerwa iko katika Mkoa wa Kagera ambapo matangazo ya Redio yanapatikana kupitia mtambo wa TBC ulioko katika Manispaa ya Bukoba ambao unasafirisha mawimbi ya Redio katika maeneo mbalimbali ya mkoa huo.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents