Serikali yaikana historia ya uhuru wa Zanzibar

SERIKALI imepiga marufuku usambazaji wa santuri ya kisasa (DVD) kwa ajili ya utalii ambayo waligawiwa wabunge, kwa maelezo kwamba imepotosha historia ya Zanzibar.

Na Mwandishi Wa Mwananchi, Dodoma


 


SERIKALI imepiga marufuku usambazaji wa santuri ya kisasa (DVD) kwa ajili ya utalii ambayo waligawiwa wabunge, kwa maelezo kwamba imepotosha historia ya Zanzibar.

Uamuzi huo umetolewa siku chache, baada ya sakata hilo kuibuliwa bungeni na Mbunge wa Dimani, Hafidh Ali Tahir (CCM), akidai kuwa Zanzibar haikupata Uhuru mwaka 1963 kama inavyoelezwa kwenye santuri hiyo, bali ni mwaka 1964 yalipofanyika mapinduzi halali.

Akitangaza uamuzi huo nje ya Ukumbi wa Bunge mjini hapa jana, Waziri wa Maliasili na Utalii, Shamsa Mwangunga, alikiri kuwa santuri hiyo ina kasoro.

Mwangunga alifafanua kwamba, kitu kibaya kilichomo kwenye santuri hiyo, ni kupotoshwa kwa tarehe ya Uhuru wa Visiwa vya Zanzibar.

Alisema ni kweli kuwamba, kuna uhuru ambao visiwa hivyo vilipata mwaka 1963 kwa amri ya wakoloni, lakini unaofahamika katika vitabu vya historia ni wa Janurai 12,1964 baada ya Mapinduzi halali ambayo yalimkomboa Mwafrika.

Waziri huyo alisema kutokana na kasoro hiyo, wizara imeamua kupiga marufuku usambazaji wake hadi zitakaporekebishwa.

“DVD ina kasoro ambayo kweli inapotosha historia ya Zanzibar. Ni kweli kuna uhuru ambao unaelezwa kwamba ulipatikana mwaka 1963, hii ipo hata katika nchi nyingine, lakini pia huwa kuna uhuru kamili na wa kweli kwa watu”, alisema na kuongeza:

“Kwa upande wa Zanzibar, uhuru wa kweli unafahamika kwamba ulipatikana baada ya Mapinduzi ya Januari 12,1964.”

Alisema ni makosa kuzungumzia Uhuru wa Zanzibar bila kutaja Mapinduzi ya Januari 12, 1964.

Alisema jana aliomba kutoa tamko la serikali bungeni, lakini bahati mbaya haikuweza kufanyika hivyo na kubainisha kuwa huenda ombi hilo likakubaliwa leo.

“Tulikuwa tutoe tamko leo (jana) bungeni, lakini hatukutajwa, lakini tumezungumza na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Bunge), huenda tukatoa tamko leo jioni (jana) au kesho (leo),” alisema na kuongeza:

“Kwa kifupi ni kwamba DVD ina kasoro, tunawaomba radhi Watanzania na tumepiga marufuku isisambabzwe hadi irekebishwe,” alisisitiza.

Sakata hilo liliibuliwa na Tahir wiki iliyopita baada ya kutaka mwongozo wa Spika, kuhusu hatua ya wabunge kusambaziwa santuri hiyo ambayo imepotosha historia ya Jamhuri ya Muungano na tarehe ya uhuru wa Zanzibar na kufanya baadhi ya wabunge wa Chama cha Wananchi (CUF), kuisaka kwa udi na uvumba ili waismabzae duniani.

Kutokana na ombi hilo, Spika Samwel Sitta, aliahidi kulishughulikia na wiki iliyopita alitangaza kwamba, Ofisi ya Waziri Mkuu ilieleza serikali ingetoa tamko jana.

Santuri hiyo ambayo iliandaliwa na Mamlaka ya Hifadhi ya Taifa (TANAPA), ilisambazwa kwa wabunge kwa ushirikiano kati ya Ofisi ya Bunge na Wizara ya Maliasili na Utalii.

Historia ya visiwa vya Zanzibar ambayo ambayo awali ilitawaliwa na Sultan, iina utata kuhusu tarehe halisi ya kupata uhuru wake. Baadhi ya wachambuzi wa mambo ya kisiasa wanaamini kuwa, utata wa historia hiyo ni moja ya kikwazo cha Mwafaka wa kisiasa kutokana na kila upande kuamii tarehe tofauti ya kupatikana kwa uhuru wa visiwa hivyo.

Wapemba wengi wenye asili ya Kiarabu wanaamini kuwa uhuru a visiwa hivyo ulipatikana 1963 chini ya uongozi wa Waziri Mkuu, Mohamed Shamte wa Chama cha Zanzibar Nationalist(ZNP).

Hata hivyo, Waunguja wengi ambao wana asili ya Afrika, wanaamini mapinduzi ya Januari 12, 1964 yaliondoa utawala wa Shamte, ambaye alidaiwa kuwa kibaraka wa Waarabu ambao walikuwa na ngome zaidi Pemba, ndiyo ilikuwa tarehe kamili ya uhuru wa visiwa hivyo.

Kutokana na hali hiyo, baadhi ya Wapemba wanaamini kuwa kilichofanyika mwaka 1964 ni mapinduzi haramu dhidi ya utawala halali wa Zanzibar.


 


Source: Mwananchi

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents