Habari

Serikali yamtaka Mbowe aombe radhi

SERIKALI ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imemtaka Mwenyekiti wa CHADEMA, Bw. Freeman Mbowe, kufuta kauli zake na kuwaomba radhi Watanzania.

Na Mwandishi Wa Majira


SERIKALI ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, imemtaka Mwenyekiti wa CHADEMA, Bw. Freeman Mbowe, kufuta kauli zake na kuwaomba radhi Watanzania.


Taarifa ya Serikali iliyotolewa jana na Waziri wa Habari, Utamaduni na Michezo, Bw. Muhammed Seif Khatib, ilikariri kauli za Mwenyekiti huyo zilizokaririwa na gazeti la Tanzania Daima Julai 4 mwaka huu.


“Aliwakashifu viongozi wa CCM na Serikali kuwa ‘ni wakoloni weusi ambao madhara ya uongozi wao ni mabaya kuliko ya wakoloni weupe walioondolewa zaidi ya miaka 40 iliyopita’,” taarifa hiyo ilimkariri Bw. Mbowe.


Katika kauli nyingine ambayo Serikali imesema inaweza kutafsiriwa kuwa ni uchochezi wa wananchi dhidi ya Serikali ni iliyosema: “Tumezoea kuchekeana, lakini ipo siku tutafanyiana kweli hadi kieleweke. Tuko tayari kwa mapambano na wakati wowote wake zetu wanaweza kuwa wajane.”


Taarifa ilisema Serikali imeshitushwa na kufadhaishwa sana na kauli hizo kutoka kwa kiongozi msomi wa chama, ambaye wananchi kwa hakika wanamtarajia kujua historia ya nchi hii na mafanikio makubwa yaliyopatikana katika kipindi cha miaka 45 ya uhuru wa Tanzania Bara.


Ilisema Bw. Mbowe anawaona Watanzania kuwa wajinga wasiojua viongozi wanaowakilisha maslahi yao na kwamba Tanzania haijapiga hatua yoyote ya maendeleo tangu uhuru.


Taarifa ya Serikali imetoa mifano ya sekta za elimu, afya na barabara, kama sehemu ya juhudi za viongozi wa Serikali katika kuondoa kero zinazowakabili wananchi na kuwaletea maendeleo.


“Baadhi ya mifano kwa upande wa elimu ni kuongezeka kwa idadi ya wanafunzi wa shule za msingi za Serikali kutoka 518,663 mwaka 1962 hadi 7,476,650 mwaka jana…walimu 10,273 mwaka 1962 hadi 148,607 mwaka jana,” ilisema taarifa.


Kuhusu sekondari, taarifa ilitoa takwimu ya shule 14,175 mwaka 1962 hadi 490,492 mwaka jana, huku walimu wakiongezeka kutoka 789 mwaka huo hadi 15,822.


“Hivi sasa Tanzania ina vyuo vikuu, vyuo vikuu vishiriki na vyuo vya elimu ya juu vipatavyo 49 vyenye wanafunzi 97,321…mwaka 1962 kulikuwa na hospitali 99, zahanati 990 na vituo vya afya vipatavyo 46, mwaka jana kulikuwa na hospitali 219, zahanati 4,679 na vituo vya afya vijijini 418,” ilisema taarifa.


Pia ilitoa takimu kuhusiana na maendeleo katika sekta ya barabara ambapo pia ilionesha kupata maendeleo makubwa kwa kipindi hicho hicho.


“Serikali na wananchi wa Tanzania wanawatarajia viongozi kama Bw. Mbowe kuzingatia angalau kanuni za msingi za uungwana na kunena ukweli…hawamtarajii kiongozi mwenye dhamana ya kuongoza chama, kuungana na watu wasioitakia mema nchi hii katika kupotosha na kuikashifu historia ya nchi, tena katika mikutano ya hadhara,” ilisema taarifa hiyo.


Source: Majira

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents