Serikali yaombwa kutatua sakata la kiwanda cha Dangote
Serikali imetakiwa kukaa na mmiliki wa Kiwanda cha Saruji cha Dangote, Aliko Dangote, kutafuta ufumbuzi wa changamoto zinazokikabili kiwanda hicho kwa kuwa anaweza kuwa balozi wa wawekezaji nchini.
Katibu wa CCM Mkoa wa Mtwara, Shaibu Akwilombe ametoa ombi hilo Jumatano hii akisema Dangote ana jina kubwa, iwapo kungekuwa na mazingira mazuri ya uwekezaji angesaidia kuwavutia wengine.
“Siku za hivi karibuni kumekuwa na taarifa kadhaa katika vyombo mbalimbali vya habari zinazohusiana na kiwanda cha Dangote, kutozalisha kwa kile kinachoelezwa ni kutokana na hitilafu za ufundi. Kwa kuwa tatizo la ufundi limejitokeza kipindi ambacho tayari kulikuwa na malalamiko kutoka kwa wamiliki juu ya gharama za uzalishaji, inasababisha kuwapo mkanganyiko kujua kiini cha tatizo,” alisema Akwilombe.
Ni wiki kadhaa sasa tangu kiwanda hicho kisitishe uzalishaji.
BY: EMMY MWAIPOPO
CHANZO: MWANANCHI