Habari

Serikali yataka Profesa Mahalu awekwe rumade

MKURUGENZI wa Mashitaka (DPP) amewasilisha ombi Mahakama Kuu Dar es Salaam kutaka kutengua masharti ya dhamana ya kesi ya kuhujumu uchumi na kuisababishia Serikali hasara ya takriban Sh bilioni tatu inayomkabili aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Italia, Profesa Costa Mahalu

Rehema Isango


MKURUGENZI wa Mashitaka (DPP) amewasilisha ombi Mahakama Kuu Dar es Salaam kutaka kutengua masharti ya dhamana ya kesi ya kuhujumu uchumi na kuisababishia Serikali hasara ya takriban Sh bilioni tatu inayomkabili aliyekuwa Balozi wa Tanzania nchini Italia, Profesa Costa Mahalu na wenzake wawili.


Eliezer Feleshi, jana aliieleza HabariLeo kuwa ofisi yake imepeleka ombi hilo ili mahakama iangalie usahihi wa masharti ya dhamana yaliyotolewa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam kwa washitakiwa wa kesi hiyo.


Katika kesi hiyo ya Jinai ya kuhujumu uchumi iliyofikishwa mahakamani hapo mara ya kwanza Januari 23 mwaka huu, washitakiwa walifikishwa hapo chini ya ulinzi wa Taasisi ya Kuzuia Rushwa (PCB), walipewa dhamana ya kusaini hati ya Sh milioni tano kila mmoja na wadhamini wawili kwa kiasi hicho hicho.


Masharti mengine yaliyotolewa katika dhamana hiyo ni kwa washitakiwa kuwasilisha hati zao za kusafiria mahakamani na kutakiwa kutotoka nje ya Dar es Salaam bila kibali. Hata hivyo, mara baada ya kufikishwa mahakamani na kupewa dhamana, baadhi ya wataalamu wa sheria walizungumza kuwa sharti la kulipa milioni tano lililotolewa kwa washitakiwa na wadhamini wao ni jepesi ikilinganishwa na kesi wanayokabiliwa nayo.


Walisema kwa mujibu wa Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA) ya mwaka 1985 kifungu cha 148, Mahakama ilipaswa kutoa sharti la kulipa taslimu ya nusu ya fedha zinazodaiwa kuibwa na washitakiwa.


Wengine wanaokabiliwa na mashitaka sita ya kuhujumu uchumi na kusababisha hasara ya zaidi ya Sh bilioni tatu (Euro 2, 065, 827) kwa Serikali ni aliyekuwa Mhasibu Steward Migwano na Mtawala Grace Martin katika Ubalozi wa Tanzania, Italia. “Maombi hayo yalipokewa na Mahakama Kuu Aprili 4 na kimsingi yanalenga kuiomba Mahakama kutazama upya mambo ya kisheria yanayohusiana na dhamana ya kesi hii,” alisema DPP.


Alifafanua kuwa, Mahakama Kuu ndiyo itakayoangalia masharti hayo ya dhamana hiyo kulingana na kosa lenyewe na kuona kama itayasahihisha au itaona ni sawa kuyaacha kama yalivyo hivi sasa.


Mapema, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ambako kesi hiyo jana ilipangwa kuanza kusomwa, maelezo ya awali baada ya upelelezi wake kukamilika mwezi uliopita ilielezwa kuwa jalada lilikuwa Mahakama kuu. Hakimu Mkuu Mkazi Mfawidhi, Sivangilwa Mwangesi alisema haelewi sababu za kuitwa kwa jalada hilo Mahakama Kuu.


Kwa upande wake, DPP alieleza hakuwa na taarifa kama hatua ya kuitwa kwa jalada hilo Mahakama Kuu inahusiana na kushughulikiwa kwa ombi lililowasilishwa na ofisi yake au kulikuwa na hatua nyingine za kisheria.


“Mimi siwezi kujua kama kupelekwa kwa faili hilo Mahakama Kuu ni kwa ajili ya ombi lililowasilishwa na Ofisi yangu au kuna suala lingine kuhusiana na kesi hii,” alisema DPP na kuongeza kuwa, hivi sasa anasubiri waraka maalumu wa kuitwa na Mahakama (summon) baada ya kuwasilisha ombi lake hilo. Hata hivyo, DPP hakutaka kuzungumzia kwa undani suala hilo kwa kuwa tayari lipo mbele ya Mahakama ambako sheria inachukua mkondo wake.


Source: Habari Leo

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents