Habari

Serikali yatenga Sh8 bilioni kwa safari za viongozi nje

IMEELEZWA kuwa safari za nje za viongozi wakuu wa serikali akiwamo rais, zitaigharimu Tanzania kiasi cha Sh8 bilioni 8 mwaka huu.

Na Mwandishi Wa Mwananchi, Dodoma


IMEELEZWA kuwa safari za nje za viongozi wakuu wa serikali akiwamo rais, zitaigharimu Tanzania kiasi cha Sh8 bilioni 8 mwaka huu.


Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Casmir Membe, alisema juzi jioni wakati akijibu hoja za wabunge kuwa kiasi hicho kimepangwa kupitia bajeti ya 2007/08.


Awali, Kiongozi wa Upinzani Bungeni, Hamad Rashid Mohammed (Wawi-CUF), alihoji ni kiasi gani cha fedha zimetengwa kwa safari hizo.


Membe alisema kiasi hicho kimetengwa kwa kuzingatia aina ya safari ambazo viongozi hao hufanya nje zikiwamo za kuhudhuria mikutano kama ya Umoja wa Mataifa au ule wa Afrika (AU).


Alisema safari za nje za viongozi zimekuwa na manufaa kwa kuweza kuiingiza nchi mapato kupitia uwekezaji au miradi na misaada kutoka nchi ambazo viongozio hao hutembelea mara kwa mara.


Mapema hamad Rashid alihoji itifaki inayofuatwa na kumtambulisha Rais wa Zanzibar anaposafiri nje ya nchi, ambako Membe alisema rais huyo anatambuliwa na kuheshimiwa kikatiba, jambo ambalo halikiuki itifaki kimataifa.


Alisema rais huyo pia anaweza kualikwa kama kiongozi wa chama, akiwa Makamu Mwenyekiti wa CCM, ambayo akienda nchi kama China, Korea Kaskazini au Cuba anaheshimiwa kulingana na itikadi.


Kuhusu hoja ya Janet Kahama (Viti Maalum CCM) aliyependekeza mjusi mkubwa wa Tanzania aliyehifadhiwa makumbusho nchini Ujerumani na jinsi gani Tanzania inanufaika na fedha za utalii, Membe alisema kuwa mipango inaendelea kumrejesha nchini kwa kushirikiana na mashirika kama Unesco.


Awali, Fatma Mikidadi (CCM-Viti Maalum) alihoji mjusi huyo wa pekee (dinosaur) aliyechukuliwa kutoka Lindi wakati wa ukoloni atarejeshwa lini nchini.


Membe alisema mjusi huyo wa pekee, alikuwa na urefu wa mita 22 na mifupa yake imehifadhiwa vizuri na kuwa kivutio cha utalii.


Source: Mwananchi

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents