Habari

Serikali yatoa neno kuhusu matokeo ya sensa zinazofanyika nchini

Waziri wa Mifugo na Uvuvi,Luhaga Mpina amewataka Watanzania kutumia takwimu za sensa mbalimbali zinazotolewa na ofisi ya Taifa ya Takwimu ili kuongeza tija na hatimaye kupunguza umasikini nchini.

Mpina ametoa wito huo leo Jijini Dodoma, alipokuwa akizindua matokeo ya utafiti wa Kilimo wa mwaka 2016/2017 ukiwa ni utafiti wa pili kufanyika nchini ambapo wa kwanza ulifanyika mwaka 2014/2015.

“Tunapenda kufanya sensa lakini mwisho wa siku hakuna anayetumia sensa hiyo. Huwezi kufanya mapinduzi ya kiuchumi bila ya kutumia matokeo mbalimbali ya tafiti,” alisema Mhe. Mpina.

Aliendelea kusema, matokeo ya tafiti hizo yametumika katika kupima mchango wa shughuli za kilimo katika Pato la Taifa, ambapo takwimu zinaonesha kuwa mwaka 2014 uchumi ulikuwa kwa asilimia 7.10 wakati mwaka 2017 uchumi ulikuwa kwa asilimia 7.1. Aidha mchango wa shughuli za kilimo kwa mwaka 2014 ulikuwa asilimia 28.8 wakati mwaka 2017 ulikuwa asilimia 30.1.

Vile vile amesema, matokeo ya utafiti yanaonesha kuwa zao la mahindi mwaka 2016/2017 uzalishaji wake ulikuwa tani 5,766,984 na kwa takwimu za utawala za mwaka 2017/2018uzalishaji ni tani 6,681,000. Katika mwaka 2017 ongezeko la thamani ya shughuli za kilimo cha mazao iliongezeka na kufikia shilingi trilioni 5.3 kutoka shilingi trilioni 5.1 mwaka 2016.

Mpina amesema, kwa upande wa Tanzania Baramkoa wa Mbeya umeendelea kuongoza katika uzalishaji wa zao la mahindi kwa tani 578,280 (10%) wakati Mkoa wa Morogoro umeongoza.

Aidha kwa upande wa mifugo, Tanzania Bara inaidadi ya ng’ombe 30,496,687, mbuzi 18,947,657, kondoo 5,565,468 na kuku wa asili 38,595,106 ambapo mikoa inayoongoza kwa asilimia kubwa ya ng’ombe ni pamoja na Tabora (8.7%), Mwanza (7.9%) na Manyara (7.2%). Tanzania Zanzibar ina idadi ya ng’ombe wapatao 175,314, mbuzi 107,993, kondoo 517 na kuku wa asili 1,754,786 na mikoa inayoongoza kwa asilimia kubwa ya ng’ombe kwa Tanzania Zanzibar ni Kaskazini Pemba (30.3%) ikifuatiwa na Kusini Pemba (19.9%).

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Taifa ya Takwimu, Dkt. Albina Chuwa amewaomba watumiaji wa takwimu hizo kuzitumia kwa manufaa ya kufuatilia na kutathimini mipango ya maendeleo ya sekta ya kilimo, mifugo na uvuvi na si vinginevyo.

Hata hivyo amesema, Tanzania bado ni nchi ya pili katika Bara la Afrika kwa kuwa na mifugo mingi hivyo ni dhahiri kuwa uwezo wa viwanda vya nyama hapa nchini na kuuza nyama na bidhaa zake zinazozalishwa kwa lengo la kujipatia fedha za kigeni.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents