Habari

Serikali yatoa siku 3 watanzania kutembelea mbuga za wanyama bure

Katika kuadhimisha siku ya mazingira duniani, Serikali imedhamiria kumuenzi mwasisi wa taifa, Mwl. Julius Nyerere kutokana na mchango wake mkubwa pamoja na misimamo yake katika kuhifadhi mazingira ya asili nchini kwa kutoa siku tatu kwa watanzania kutembelea bure mbuga za wanyama.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais, January Makamba (kushoto)

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), January Makamba amesema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati akizungumzia maadhimisho ya siku ya mazingira duniani yanayotarajiwa kufanyika kitaifa kuanzia Juni Mosi hadi Juni 5 katika Kijiji cha Butiama mkoani Mara, alikozaliwa, kukulia na kuzikwa Mwalimu Nyerere.

“Serikali imetoa siku tatu kuanzia Ijumaa ya wiki hii hadi Jumapili kwa Watanzania kuingia bure katika mbuga zote za wanyama nchini, lengo likiwa ni kuwaona wanyama na kutambua kuwa wako kama walivyo kutokana na kuwepo kwa mazingira. Kadhalika imeandaa mjadala wenye kutoa muongozo kuhusu mustakabali wa nchi kuhusu mazingira, wakishirikisha wataalamu mbalimbali wakiwemo viongozi wa dini kwa ajili ya kueleza umuhimu wa kuhifadhi mazingira, kwa kuwa kwa sasa hali ni mbaya nchini”,alisema January Makamba.

Katika kilele cha maadhimisho hayo, Makamu wa Rais Samia Hassan Suluhu anatarajiwa kuwa mgeni rasmi, ataongoza kupanda miti katika shamba la Mwalimu Nyerere pamoja na kuendesha kongamano la kitaifa la mazingira likishirikisha pia viongozi wengine na wanafamilia ya Nyerere huku Kauli mbiu katika maadhimisho hayo ikiwa ni “Hifadhi mazingira, Muhimu kwa Tanzania ya Viwanda”.

Kuhusu maadhimisho hayo kufanyika Butiama, January amesema inatokana na mchango mkubwa wa Mwalimu Nyerere wakati wa uhai wake akiwa mwanamazingira wa kwanza, aliyesimama thabiti na kuwa na falsafa za kuhifadhi mazingira yanayoifanya Tanzania iwe kama ilivyo kwa sasa.

Akifafanua zaidi kuhusu maadhimisho hayo, January amesema Jumamosi wiki hii litafanyika kongamano kuhusu mazingira ambapo mijadala minne inayohusu hali ya mazingira, athari za uchumi kwa sekta ya mazingira nchini katika kilimo, uvuvi, ufugaji na utalii zitawasilishwa na majopo ya wataalamu mbalimbali.

Kuhusu kutembelea mbuga za wanyama, alisema tayari wizara yake wamezungumza na Wizara ya Maliasili na Utalii na Mamlaka ya Hifadhi ya Taifa (Tanapa) ili Watanzania waingie katika mbuga hizo kwa siku tatu bure, lengo likiwa ni kuona uwepo wa wanyama na kujifunza kuwa mazingira yanahitaji kulindwa zaidi.

By Godfrey Mgallah

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents