Siasa

Serikali yawakana wanafunzi Ukraini

Serikali imesema haiwatambui wanafunzi 29 walioko Ukraini na haitahusika kwa lolote linalowasibu, kwani walikwenda huko kwa ufadhili binafsi…

Wanafunzi walioko Ukraini


Na Rabia Bakari


SERIKALI imesema haiwatambui wanafunzi 29 walioko Ukraini na haitahusika kwa lolote linalowasibu, kwani walikwenda huko kwa ufadhili binafsi.


Akizungumza na waandishi wa habari Dar es Salaam jana, Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia, Bw. Selestin Gesimba, alisema awali wanafunzi hao waliiomba Serikali iwasaidie kupata mikopo ya masomo nje ya nchi na wakajibiwa kuwa hakuna fedha za kuwakopesha.


Alisema Serikali iliwashauri watafute nafasi katika vyuo vya elimu ya juu nchini, lakini kwa uamuzi wao, walijilipia nauli na kwenda Ukraini bila idhini ya Serikali wala ahadi ya maandishi kuonesha kuwa wangesaidiwa na Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu.


“Kwa kuwa wazazi wa wanafunzi hao waliamua kwa nia njema kuwapatia watoto wao elimu ya juu nje ya nchi kwa gharama binafsi, wanawajibika kugharimia masomo ya watoto wao.” alisema Bw. Gesimba.


Aliongeza kuwa Serikali ina utaratibu wa kutoa ufadhili kulingana na makubaliano na nchi rafiki kama vile China, Urusi, Polandi na zingine za Jumuiya ya Madola kwa masharti tofauti.


Aliyataja baadhi ya masharti ni kuwa aliyechaguliwa alipie gharama za nauli ya kwenda na kurudi baada ya kumaliza masomo na matibabu.


Wanaobainika kuwa na uwezo mdogo, hushauriwa kuomba mkopo kutoka Bodi ya Mikopo.


Alisema kuna wanafunzi wanaopelekwa na Serikali kwa utaratibu wa ufadhili na nchi rafiki na wanaopelekwa kusoma kozi maalumu za kipaumbele kwa maendeleo ya nchi, ambazo hazipatikani nchini au zinapatikana kwa uchache.


Aidha alisema wanafunzi wanaopelekwa na wazazi wao au mashirika yasiyo ya kiserikali ndilo kundi la udhamini binafsi.


Alisema katika mwaka wa masomo 2005/06, wanafunzi 130 walipata ufadhili katika vyuo vikuu mbalimbali Ukraini na kati yao, 84 tu ndio waliokamilisha taratibu za kuondoka nchini na kupata mkopo wa Bodi ya Mikopo na wengine 46, hawakukamilisha taratibu hizo, hivyo hawakuondoka.


Aliongeza kuwa katika mwaka wa masomo 2006/07, wanafunzi hao walishauriwa wajiunge na vyuo nchini kwa kuwa Serikali haikuwa na uwezo wa kuwakopesha wanafunzi wapya nje ya nchi.


Wanafunzi 17 kati yao walikubali kufanya hivyo na mpaka sasa wanaendelea na masomo yao katika vyuo mbali mbali nchini.


Aliongeza kuwa wanafunzi 29 wenye matatizo Ukraini ni kati ya 46 waliokataa ushauri wa Serikali na kuamua kwa utaratibu wao binafsi kwenda huko.


Alisema wanafunzi hao ambao wamekwama kulipa ada na kusimamishwa masomo, wamekuwa wakiushinikiza Ubalozi wa Tanzania mjini Moscow, Urusi, uiombe Serikali iwasaidie, lakini Serikali imeshindwa kufanya hivyo kwa sababu haikutenga fedha kwa ajili yao.


Aliongeza kuwa baada ya kuona ombi lao halifanikiwi, wanafunzi hao walikwenda Ubalozi wa Uingereza mjini Moscow na kupiga kambi wakiomba Serikali ya Uingereza iwasaidie, kwa kuwa Serikali ya Tanzania imeshindwa kufanya hivyo.


Alisema Serikali haiwajibiki na gharama zinazojitokeza kwa wanafunzi walio nje ya nchi kwa udhamini binafsi kwa sababu ya ufinyu wa bajeti.


Aliwataka wanafunzi hao kuondoka mara moja katika Ubalozi wa Uingereza na kurejea vyuoni kwao kuendelea na masomo kwa gharama zao.


Alisema wakishindwa kufanya hivyo, warejee nchini haraka ili waanze utaratibu wa kujiunga na masomo katika vyuo vya nchini.


Alisema wale ambao hawana nauli watajaza fomu maalumu kuomba mkopo wa nauli na watakaporejea nchini, wafanye utaratibu wa kurejesha mkopo huo mara moja.


Bw. Gesimba alisema Serikali haihusiki na matatizo yoyote ya wanafunzi hao ikiwa ni pamoja na kuchunguzwa na vyombo vya usalama, kunyang’anywa hati za kusafiria na kufunguliwa mashitaka ya uhalifu, kama ilivyoelezwa na baadhi ya wazazi wa wanafunzi hao.


Mbali na matatizo hayo, wanafunzi hao wanakabiliwa na madeni katika vyuo walivyokuwa wanasoma, ya ada na matumizi mengine ambapo inadaiwa kuwa hawataruhusiwa kuondoka nchini humo hadi watakapolipa madeni hayo.


Alipoulizwa kuhusu hofu ya wanafunzi hao kushindwa kulipa deni la tiketi watakazotumiwa watakaporudi na kuisababishia Serikali hasara, Bw. Gesimba alisema Serikali inaamini kuwa kama kweli wana nia ya kurejea watafanya kila njia kurejesha pesa hizo.


Juzi, Umoja wa Vyama vya Upinzani, ulichanga jumla ya sh. milioni moja kama mchango wa dharura kwa ajili ya kuwasaidia wanafunzi hao.


Katika tamko lao la pamoja mbele ya waandishi wa habari, walisema wamefikia uamuzi huo, baada ya kupata taarifa za kusikitisha kuwa wanafunzi hao wanakabiliwa na matatizo makubwa na wamekwama kuendelea na masomo.


Wakuu hao waliiomba Serikali kufanya uungwana kuwasaidia haraka wanafunzi hao ambao wanaishi kama watoto yatima.


Waliwataka Watanzania wote kutoa misaada ya kibinadamu ili kuokoa maisha ya wanafunzi hao ambao walisema wapo katika hali mbaya.


Waliitaka Serikali ilieleze Taifa kuwa inawatambua wanafunzi hao 29 na iseme ni kwa nini vijana hao wametelekezwa wakati waliondoka nchini kwa baraka zote za Serikali wakiahidiwa kutumiwa fedha mara watakapoanza masomo yao lakini Serikali haikufanya hivyo.


Walimtaka Waziri wa Elimu ya Juu, Sayansi na Teknolojia Profesa Peter Msolla ajiuzulu kwa madai kwamba ameshindwa kumsaidia Rais Jakaya Kikwete katika suala hilo.


Viongozi waliokutana ni pamoja na Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, Bw. Augustino Mrema (TLP) na Bw. James Mbatia, NCCR -Mageuzi.


Source: Majira

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents