Habari

Serikali yawakumbusha wasanii kurasimisha kazi zao

Serikali imetoa wito kwa wasanii nchini kurasimisha kazi zao ili kuweza kutambulika, kupata haki zao na kuongezea pato lao na la taifa.

Wito umetolewa leo jijini Dar es Salaam na Naibu Waziri Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Mhe.Anastazia Wambura wakati wa Mkutano na waandishi wa habari ulikuwa unahusu ubunifu wa vipaji na jinsi ya kuviendeleza.

“Sanaa inaongeza uelewa, sanaa ni chanzo kikubwa cha ajira hasa kwa vijana inayopelekea kukua kwa pato la taifa ingawa kuna changamoto kwa wasanii kutojitokeza au kujisajili ili kuweza kutambulika katika jamii”, alifafanua Naibu Waziri Wambura.

Alisema kuwa ili kutekeleza agizo la Rais wakati wa hotuba ya uzinduzi wa Bunge kuhusu haki za wasanii nchini, Wambura aliwataka wadau mbalimbali wa sanaa na sekta binafsi kushirikiana na Serikali katika kuhakikisha maslahi ya wasanii yanaboreshwa na kupinga uharamia wa kazi za wasanii.

Aidha, Wambura aliwataka wasanii kufuata Sheria, Kanuni na taratibu kwa kushirikiana na taasisi zinazohusika na masuala ya sanaa ikiwemo Tasuba, Basata, Cosota, Bodi ya Filamu ili kuwawezesha kufanya kazi kwa unafuu.

“Kama tunataka maendeleo ya kweli ni lazima kuthubutu, unapokuwa huna lengo au ndoto ni mkasa mkubwa katika jamii hivyo tunapaswa kuwa na ndoto zinazopelekea maendeleo yetu” alifafanua Wambura.

Kwa upande wake Rais wa Taasisi ya TCDB Mwalimu Calorus Bujimu, alisema kuwa taasisi imeandaa programu ya kukuza kazi za wasanii nchini kwa lengo la kuibua vipaji vya wasanii na kuvikuza.
Alisema kuwa uanzishwaji wa programu hiyo ni matokeo ya utafiti yaliyobaini kuwa uwepo wa wasanii wengi wenye vipaji katika Nyanja mbalimbali za sanaa, lakini wanakabiliwa na changamoto za kiuchumi na kukosa ubunifu.

NA BEATRICE LYIMO NA GEORGINA MISSAMA – MAELEZO

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents