Habari

Serikali yawarejesha kazini watumishi wa darasa la saba

Serikali imeamuru kurudishwa kazini kwa Watumishi wote ambao walikuwa na ajira za kudumu au ajira za mikataba (kwa watendaji wa Vijiji na Mitaa) au ajira za muda ambao walikuwa kazini kabla ya Mei 20, 2004 ulipoanza kutumika waraka wa Utumishi Na. 1 wa mwaka 2004 ambao umetaja kuwa cheti cha ufaulu wa mtihanai wa kidato cha nne kama sifa ya msingi kwa mtumishi wa Umma.

Kauli hiyo imetolewa leo bungeni Mjini Dodoma na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Kapteni Mstaafu George Mkuchika alipokuwa akitoa Kauli ya serikali kuhusu watumishi waliondolewa kwenye mfumo wa malipo ya mshahara kwa kukosa sifa ya cheti cha kufaulu mtihani wa elimu ya kidato cha nne.

“Watumishi wa Umma Elfu Moja Mia Tatu Sabini (1,370) waliolegezewa masharti ya sifa za muundo kupitia barua ya Katibu Mkuu Utumishi yenye Kumb. Na. CCB.271/431/01/p/13 ya tarehe 30 Juni, 2011 warejeshwe kazini mara moja, walipwe mishahara yao kwa kipindi chote ambacho walikuwa wameondolewa kazini na waendelee na ajira zao hadi watakapostaafu kwa mujibu wa Sheria,” alisema Mhe. Mkuchika.

Hata hivyo amesema kuwa uamuzi huu uliotajwa hautawahusu watumishi wawasilisha vyeti vya kughushi katika kumbukumbu za ajira zao, watumishi waliokuwepo katika ajira kabla ya tarehe 20 Mei, 2004 pamoja na warumishi wote walioajiriwa baada ya tarehe 20 Mei 2004 wakiwa hawana sifa za kufaulu mtihani wa kidato cha nne kwa kuwa walijipatia ajira kinyume cha maelekezo ya Serikali.

Aidha, watendaji wakuu wa Idara za Utawala na Utumishi wote walioshiriki kuwaajiri Watumishi wasiokuwa na sifa ya kufaulu mtihani wa kidato cha nne katika Utumishi wa Umma baada ya tarehe 20 Mei, 2004 watachukuliwa hatua za kinidhamu kwa mujibu wa sheria, kanuni za taratibu.

Vilevile watendaji wakuu na maafisa wote wanaosimamia zoezi hili ambao kwa namna yoyote ile watashiriki kuhujumu zoezi hili kwa kuondoa au kuharibu kumbukumbu za Watumishi ili haki isitendeke, watachukuliwa hatua za kinidhamu na za kijinai ikibidi.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents