Habari

Serikali yawataka Wakandarasi nchini kuwajibika

Serikali imewataka wakandarasi kuwajibika na kufanya kazi zao kwa ufanisi na weledi ili kuishawishi Serikali kuwaamini na kuwapatia zabuni za kutekeleza miradi mikubwa nchini.

Akizungumza katika ufunguzi wa Mkutano wa 20 wa Mashauriano ya Bodi ya Makandarasi (CRB), mjini Dodoma, Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, amesema kuwa miradi mingi mikubwa nchini imekuwa ikitekelezwa na Makandarasi kutoka nje ya nchi hali inayopelekea Serikali kutumia fedha nyingi kuwalipa Makandarasi hao.

“Muda umefika sasa kwa makandarasi wazawa kuungana na kuomba zabuni za kutekeleza miradi mikubwa itakayowajengea uwezo kama ujenzi wa bomba la Mafuta kutoka Uganda hadi Tanga, Reli ya Kisasa na miradi mingine.” amesema Makamu wa Rais.

Aidha, amefafanua kuwa kutekelezwa kwa miradi hiyo na Makandarasi wazawa kutaokoa fedha za ndani za watanzania na hivyo kupelekea fedha hizo kubaki nchini na vijana kupata ajira.

Sambamba na hilo Makamu wa Rais amewasisitiza Makandarasi hao kuwa wa kwanza kuomba zabuni pindi zinapotangazwa kwani Serikali ya Awamu ya Tano itatoa kipaumbele kwa Makandarasi wazawa wote nchini.

Makamu wa Rais ameitaka CRB kuhakikisha inasimamia Makandarasi hao kutekeleza miradi kwa muda uliopangwa pamoja na kufuata maadili katika utendaji wao wa kazi.

Kuhusu suala la ulipaji wa madeni ya Makandarasi Mhe. Samia Suluhu Hassan amesema kuwa kwa sasa Serikali inendelea kufanya uhakiki wa madeni hayo ambapo zoezi la malipo litaanza mara baada ya uhakiki huo kukamilika.

Kwa Upande wake, Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Profesa Makame Mbarawa amesema kuwa kutokana na umuhimu wa kuwathamini Makandarasi wazawa Wizara imetenga miradi maalum kwa ajili ya kuwajengea uwezo Makandarasi hao.

“Makandarasi msisite kuomba zabuni pindi zinapotangazwa, naahidi nitasimamia kwa uaminifu na kuhakikisha kila mkandarasi mwenye sifa anapata zabuni kwa mujibu wa sheria”, amesema Profesa Mbarawa.

Naye, Mwenyekiti wa Bodi ya Usajili wa Makandarasi nchini, Eng. Consolata Ngimbwa amemhakikishia Makamu wa Rais kuwa watatumia mkutano huo kujadili changamoto zinazowakabili na hivyo kuja na mapendekezo sahihi ya kutatua changemoto hizo.

Mkutano huo wa siku mbili wenye kauli mbiu isemayo “Miaka 20 ya CRB, utendaji wa Makandarasi unaozingatia maadili na Sheria kama mkakati wa kuaminiwa na waajiri” una lengo la kuwakutanisha makandarasi wa ndani na nje ya nchi kwa lengo la kujadili kwa pamoja changamoto zao na kuzitafutia ufumbuzi.

Imetolewa na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano.

Na Emmy Mwaipopo

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents