Habari

Serikali yazitaka halmashauri kuongeza ukusanyaji wa kodi ya pango la ardhi

Serikali imezitaka Halmashauri nchini kuimarisha ukusanyaji kodi hususani katika pango la ardhi na kuachana na kodi ndogondogo ili kuweza kujiendesha zenyewe katika shughuli mbalimbali za maendeleo.

Akizungumza na watumishi wa Manispaa ya Ubungo Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. Angelina Mabula alisema kuwa katika mfumo mpyawa kielekitroniki ambao kwa sasa umewekwa katika Idara ya ardhi kwa lengo la kodi ya pango la ardhi, ni mfumo rahisi kwa Manispaa zote nchini.

“Bajeti yenu ni ndogo ukilinganisha na wadaiwa sugu kwa Manispaa yenu mnawadai milioni 500 kwa block ya kimara tu, mnaviwanja 2,1210 kwa hiyo mkidai kwa Manispaa nzima mnaweza kupata pesa nyingi ambayo itawezesha shughuli za Halmashauri kusonga mbele”, alisema Mhe. Mabula.

“Fedha zote ziko kwenye Idara hii ya ardhi kiasi kwamba mkiweza kusimamia zoezi la ukusanyaji pango la ardhi na utoaji wa hati kwa kufuata utaratibu sahihi, fedha hiyo ingeweza kuleta mapato mengi sana”, alisisitiza Mhe. Mabula.

Aidha Naibu Waziri Mabula aliwataka watendaji wa Manispaa hiyo kuhuisha Mabaraza ya Ardhi ya Kata na kuwapa elimu kuhusu masuala ya migogoro ya ardhi, ambapo pia aliwashukuru kwa kuweza kutatua migogoro 37 ya ardhi katika Manispaa ya Ubungo kiasi ambacho wanaonyesha kuwa na mwelekeo katika kutatua migogoro ya ardhi kwa haraka.

Katika ziara yake ya kikazi inayoendelea katika Mkoa wa Dar es Salaam Waziri Mabula aliwataka watendaji wa Manispaa hiyo kuhakikisha wadaiwa sugu wapatao 300 wanafuatiliwa na kulipa madeni yao ili kuongeza mapato yatakayosaidia kuendesha shughuli za manispaa ikiwemo kulipa mishahara ya watumishi, kulipa fidia kwa maeneo wanayohitaji kuyatwaa kwa shughuli za Manispaa.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents