Habari

Shigongo amshangaa! Mh. Lissu

Mwandishi wa vitabu na mfanyabiashara maarufu nchini, Eric Shingongo ameshangazwa na Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu huku akisema anamheshimu sana mbunge huyo lakini anashindwa kumwelewa kwa kitu kimoja kwamba kwa nini hawezi kukubali pale jambo jema linapofanyika.

Shigongo amehoji kuwa kwanini Mwanasheria huyo amekuwa ni mpingaji wa mambo mazuri na kusema jambo hili linamshushia heshima.

Kwanza kabisa nimshukuru Mungu kwa kuendelea kuisimamia amani ya nchi yetu mpaka muda huu.
Pili niwashukuru Watanzania wenzangu kuwa na moyo wa uvumilivu ambao wameendelea kuuonyesha wakati nchi yetu ilipita katika kipindi cha mpito kiuchumi, matumaini yangu ni kwamba si muda mrefu viongozi wetu watajifunza jambo katika kinachoendelea na hatimaye mambo yatabadilika na kuwa mazuri, hili ndilo tumaini langu.
Baada ya kusema hayo, hebu sasa nami niunge kidogo juu ya kinachoendelea hapa nchini juu ya sakata la madini.
Ndugu zangu, tunashinda vita hii, Rais Magufuli angefanya nini zaidi ya kilichofanyika? Akae kimya tuendelee kuibiwa? Hapana! Ilikuwa ni lazima kuchukua maamuzi magumu ambayo hatimaye yamewaleta Barrick na Acacia mezani. HONGERA MHESHIMIWA RAIS, WAZALENDO WATAKUUNGA MKONO.
Namheshimu sana Lissu, sana tu. Ni msomi wa sheria, tena mzuri tu! Lakini namshangaa, nashindwa kumwelewa kwa kitu kimoja kwamba kwa nini hawezi kukubali pale jambo jema linapofanyika?
Mimi nadhani ni kujijengea heshima kubwa sana kuonyesha uzalendo pale nchi inapopambana na wizi wa maliasili ambazo hata hao Acacia wenyewe wameukubali, sasa kwa nini Lissu anaendelea kubeza kile kinachofanyika? Hakika hili linamshushia heshima.
Rais amezuia mchanga usisafirishwe nje kwa faida ya Watanzania, rais amegundua tunaibiwa sababu ya sheria mbovu za madini, ameagiza zirejeshwe bungeni kujadiliwa upya, jambo ambalo huko nyuma halikufanyika.
Juhudi za rais zimefanya kiongozi wa Barrick alazimike kuja nchini kubembeleza yaishe na wapo tayari kulipa. Tumefika hapa kwa juhudi za rais jasiri, amefanya kwa faida ya wote.
Kuna haja gani ya kumbeza? Ushauri wangu kwa ndugu yangu, Lissu na Watanzania wenzangu ni kuunga mkono pale mema yanapofanyika na kupinga pale mabaya yanapotendeka, hii ndiyo heshima na uzalendo badala ya kupinga kila kitu.
Wazungu wana msemo ‘Silence is Wisdom’ yaani (Ukimya ni Hekima), namshauri ndugu yangu Lissu anyamaze au aweke pembeni itikadi na kuweka TAIFA LETU MBELE.
E.J SHIGONGO.

Na Emmy Mwaipopo

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents