Siasa

Shy-Rose atangaza nia Kinondoni

Shy-Rose Bhanji ametangaza nia ya kugombea ubunge katika jimbo la Kinondoni kwa kupitia Chama Cha Mapinduzi, alisema lengo lake kubwa ni kuwa kiungo muhimu katika jamii ya wana Kinondoni wote na si kuwa mwakilishi kama ambavyo imekuwa ikieleweka na kuzoeleka.

“Neno ubunge linastahili tafsiri mpya kabisa … mbunge anatakiwa kuwa kiungo cha jamii badala ya kuwa mwakilishi wa jimbo, ili kuendana na wakati na matatizo ambayo yanawakabili wananchi,” alisema Bhanji.

Alisema hata sifa za mbunge nazo zinatakiwa kubadilika kutokana na mabadiliko ya majukumu, kwani anastahili kuwa mhamasishaji, kiungo na kufanya kazi usiku na mchana, lakini awe pia na ofisi katika kila kata jimboni.

Kada huyo alisema sera yake ni kushirikisha kila mwananchi wa Kinondoni kuleta maendeleo kwa kila mmoja kutoa maoni, mawazo na mchango akihakikisha hata asiye na uwezo “abebe tofali kutoka upande mmoja kwenda sehemu husika”.

Alisema atapigania kwa ari zaidi, nguvu zaidi na kazi zaidi elimu, afya, ajira kwa vijana, vita dhidi ya dawa za kulevya kwa vijana na haki za wasanii na wajane katika kujikwamua kiuchumi na kuleta msukumo mpya katika uhusiano wa kijamii.

Kuhusu kujitokeza kwake, alisema kumetokana na kauli za Rais Jakaya Kikwete za kutaka wanawake wajitokeze kuwania uongozi ili Tanzania ifikie uwiano wa asilimia 50 kwa 50 baina ya wanawake na wanaume katika kufikia uamuzi.

Bhanji amepata kuwa mwandishi wa habari wa magazeti ya Serikali ya Daily News, mtangazaji wa Televisheni ya Taifa (TBC1), Meneja Uhusiano Shirika la Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (Dawasco) na Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano cha Benki ya NMB tangu mwaka 2006 hadi leo.

Jimbo la Kinondoni hivi sasa linawakilishwa na Iddi Azzan ambaye pia ni kada wa CCM.

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents