Habari

Siasa imevamiwa na wafanyabiashara wezi

Baadhi ya wafanyabiashara wanakimbilia kwenye siasa kwa ajili ya kulinda maslahi yao na kuiba fedha za walipa kodi ili waendelee kuwa mamilionea.

Na Richard Makore



Baadhi ya wafanyabiashara wanakimbilia kwenye siasa kwa ajili ya kulinda maslahi yao na kuiba fedha za walipa kodi ili waendelee kuwa mamilionea.


Mkurugenzi wa Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (TAMWA), Bi. Ananilea Nkya, alitoa madai hayo jana wakati akizungumza na ujumbe wa shirika lisilo la serikali la FK kutoka nchini Norway.


Hata hivyo, Bi. Nkya alisema, wapo wafanyabiashara wachache wenye moyo wa kutumikia wananchi ambao wanaingia katika siasa kwa nia njema.


Alisema siku za hivi karibuni kumekuwa na wimbi kubwa la watu kukusanya fedha ili kununua kura ambapo lengo lao kubwa ni kutumia nafasi zao katika kipindi cha miaka mitano watakachokuwa madarakani kujilimbikizia mali.


Alisema watu wa namna hiyo wanatumia nafasi zao kushinikiza kubadilishwa kwa sera za nchi, sheria pamoja na kutumia nafasi zao kupata vitu ambavyo kama wasingekuwa viongozi wasingeweza kuvipata.


Bi. Nkya alifafanua kuwa mtu yeyote anayekusanya fedha nyingi za kununua kura za wananchi lazima atahakikisha katika kipindi cha uongozi wake anaiba sana ili aweze kuzirudisha pamoja na faida.


Alisema wanasiasa wengi wamekuwa wabinafsi ambao kila kukicha wanafikiria maslahi yao pamoja na mbinu zitakazowawezesha kuendelea kujilimbikizia mali.


“Hakuna kiongozi anayefikiria wenzake ili waweze kuwa na maisha bora kama yeye bali anajifikiria yeye mwenyewe,“ alisema.


Aidha, Bi. Nkya alilalamikia vyama vya siasa hapa nchini kwa kutowateua wanawake wengi kugombea nafasi za uongozi licha ya kuwa na sifa kama wanaume.


Alisema njia pekee itakayofanya mawazo ya wanawake yasikike na kuheshimiwa ni ile ya kuwapatia nafasi zaidi za kugombea uongozi mbalimbali.


Aliongeza kuwa TAMWA imeendelea kuwa mstari wa mbele kuwaelimisha wanawake katika kupigania haki zao jambo ambalo limefanya waamke na kuzidai.


Mkurugenzi huyo alipendekeza kuwa endapo Rais wa nchi atakuwa mwanaume basi makamu wake awe mwanamke ili kusaidia sauti zao kusikika zaidi.


Source: Nipashe

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents