Siasa

Sijiuzulu, sijaiba – Mwanyika

MWANASHERIA Mkuu wa Serikali, Johnson Mwanyika, amepuuza wito wa kumtaka kujiuzulu wadhifa huo kutokana na kuhusishwa na kashfa ya kampuni ya kuzalisha umeme wa dharura ya Richmond, akisema “milele na milele ni mtu safi.”

Mwandishi Wa Habari Leo

 

 

 

MWANASHERIA Mkuu wa Serikali, Johnson Mwanyika, amepuuza wito wa kumtaka kujiuzulu wadhifa huo kutokana na kuhusishwa na kashfa ya kampuni ya kuzalisha umeme wa dharura ya Richmond, akisema “milele na milele ni mtu safi.”

 

“Kwa wale wanaonifahamu, mimi ni mtu safi tangu nilipoanza kazi serikalini Machi 10, 1973.

 

Nendeni mkawahoji watu niliofanya nao kazi,” Mwanyika aliwaambia wahariri wa vyombo mbalimbali vya habari Dar es Salaam jana alipokuwa akizungumza kama Mwenyekiti wa Timu ya Rais ya Uchunguzi wa wizi wa fedha za Akaunti ya Madeni ya Nje (EPA) katika Benki Kuu ya Tanzania.

 

Alisema kilichoelezwa na Kamati teule ya Bunge ya kuchunguza mkataba wa Richmond siyo tuhuma, ni mapendekezo, hivyo haoni sababu yoyote ya kujiuzulu.

 

“Sioni sababu yoyote ya kujiuzulu, sijaiba,” alisema Mwanyika na kuongeza kuwa waliojiuzulu kutokana na kashfa hiyo walifanya hivyo kwa sababu ya siasa ya sehemu zao walizokuwa wakiongoza. “Mimi ni mtaalamu kama vile walivyo mawakili, anapokosea kuna taratibu zake za kumwajibisha kitaalamu. Mimi binafsi ni mtu safi, milele na milele mimi ni mtu safi.”

 

Alisema kwamba Rais Jakaya Kikwete alipoteua timu ya uchunguzi wa EPA alitaja ofisi akiwa na maana ya Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mkuu wa Jeshi la Polisi na ya Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, hivyo “Mwanyika yupo au hayupo, kazi itaendelea kama kawaida.”

 

Tangu kutangazwa hadharani kwa ripoti ya Kamati teule ya Bunge kuhusu mkataba wa Richmond na kusababisha kujiuzulu kwa mawaziri watatu, baadhi ya wanasiasa na wanaharakati, wamemtaka Mwanyika ajiuzulu baada ya ofisi yake kuhusishwa na kashfa hiyo.

 

Aliyekuwa Waziri Mkuu, Edward Lowassa, Waziri wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi na Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk. Ibrahim Msabaha, walijiuzulu nyadhifa zao kutokana na kashfa hiyo na hivyo kusababisha kuvunjwa kwa Baraza la Mawaziri, mwanzoni mwa mwezi uliopita.

 

Mbali ya Mwanyika, pia umekuwapo mwito wa kutaka ajiuzulu Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru), Edward Hosea, baada ya awali taasisi yake kudai hakukuwa na matatizo yoyote katika mkataba huo na Richmond ambayo ililetwa kuzalisha umeme wa dharura baada ya nchi kukumbwa na matatizo mwaka 2006.

 

 

 

Source: Habari Leo

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents