BurudaniHabari

Sikinde haitunyimi usingizi – Msondo

Msondo Ngoma UONGOZI wa bendi ya umesema hautishiki na fununu za kuchukuliwa baadhi ya wanamuziki wake nyota kama ambavyo uvumi huo ulivyoenea maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam.

na Abdallah Menssah

 

UONGOZI wa bendi ya Msondo Ngoma umesema hautishiki na fununu za kuchukuliwa baadhi ya wanamuziki wake nyota kama ambavyo uvumi huo ulivyoenea maeneo mbalimbali jijini Dar es Salaam.

 
Akizungumza juzi jijini Dar es Salaam, Meneja wa bendi hiyo, Said Kibiriti, alisema kuwa bendi yake haitishiki na uvumi unaoenezwa na wapinzani wao, DDC Mlimani Park ‘Sikinde Ngoma ya Ukae’, kuwa wako mbioni kuwasambaratisha kwa kuwanyakua baadhi ya nyota.

 
Kibiriti alisema Sikinde imeishiwa kimuziki ndiyo maana wamebaki kupiga porojo tu badala ya kuonyesha vitendo.

 
“Unajua bwana, sisi Msondo huwa hatuna muda wa malumbano na porojo, hapa ni muziki tu, sasa wale wenzetu wameishiwa ndiyo maana kila kukicha wanatuzushia maneno ili wapate umaarufu kupitia kwetu,” alisema.

 
Meneja huyo aliongeza kuwa bendi yake ina wanamuziki wengi na wote wana vipaji vilivyo sawa, hivyo hata kama Sikinde wakichukua nusu yao kamwe hawawezi kuyumba.

 
“Kama ni kuporwa wanamuziki na Sikinde kwetu si mara ya kwanza, wengi wamelishakwenda na Msondo bado ipo palepale,” alisema na kuongeza:

 
“Kumbuka marehemu Mwanyiro, Bichuka, na hivi juzi juzi Hussein Jumbe wamekwenda huko lakini Msondo ndiyo kwanza kumekucha.”

 
Kibiriti alijigamba kuwa licha ya upinzani huo hawana wazo hata siku moja kumchukua mwanamuziki kutoka Sikinde kama wao wanavyodhani, kwani hawajaona mwenye kiwango cha kuwavutia.

 

Source: Tanzania Daima

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents