Michezo

Simba VS Azam..Leo ndio Leo!

Klabu mbili nguli za soka jijini Dar-Es-Salaa SIMBA SC na Azam FC zinashuka dimbani kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam kumenyana katika mechi ya kuelekea msimu mpya wa ligi kuu ya soka nchini kuwania Ngao ya Jamii, iliyopangwa kuanza leo alasiri majira ya saa 10:30 jioni.

Simba inashuka dimbani ikiwa na kumbukumbu ya kuchapwa mabao 3-0 na Sofapaka ya Kenya, katika mchezo wa kirafiki, uliofanyika katika Uwanja wa Taifa siku ya alhamisi iliyopita.

Mpaka kufikia leo siku ya mchezo, timu ya Simba imeshacheza mechi tatu za kirafiki wakati ikiwa jijini Arusha ilipoweka kambi majuma kadhaa yaliyopita na kucheza mechi dhidi ya Mathare United ya Kenya, JKT Oljoro ya Arusha ambazo kila moja ilishinda 2-1, kabla ya kulazimishwa sare ya 1-1 na Sony Sugar ya Kenya.

Simba inajivunia washambuliaji wake watatu Daniel Akuffo, Phelix Sunzu na Emmanuel Okwi ambao wote wamewasili. Mchezaji Mghana Akuffor hadi sasa ameshacheza katika mechi nne za kirafiki, amefunga mabao matatu, ingawa hiyo ambayo hakufunga, dhidi ya Sofapaka hakumaliza hata nusu ya kwanza ya mchezo, baada ya kuumia na kutoka.
Simba pia inajivunia upande wa safu ya kiungo ambapo wachezaji Mrisho Khalfan Ngassa na Ramadhan Suleiman Chombo ‘Redondo’ kwa mara ya kwanza leo watacheza dhidi ya timu yao ya zamani- wote hawa waliichezea Azam ilipoifunga Simba 3-1 katika Robo Fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kagame Julai 24, mwaka huu Uwanja wa Taifa.

Azam itakayotokea Chamazi, nje kidogo ya Jiji la Dar es Salaam, itaingia uwanjani ikiwa na kumbukumbu nzuri ya kushinda mechi zake zote nne za kujipima nguvu, dhidi ya Prisons 1-0, Transit Camp 8-0, Coastal Union 2-0 na Azam Akademi 4-0.

John Bocco ‘Adebayor’ aliyefunga mabao yote matatu Simba ilipokutana na Azam mara ya mwisho na mwenye kawaida ya kufunga kila mechi baina ya timu hizo, leo kwa mara nyingine atakuwa tishio kubwa kwa Wekundu wa Msimbazi, akicheza mbele ya kiungo bora kwa sasa Afrika Mashariki, Salum Abubakar “Sure Boy Jr”.
Beki wa zamani wa Simba SC, Mganda Joseph Owino bado hajamshawishi kocha mpya wa Azam, Boris Bunjak na hapana shaka leo Said Mourad atacheza pamoja na Aggrey Morris katika beki ya kati, juu yao akisimama Jabir Aziz na Abdi Kassim ‘Babbi’ anaweza kuanza na Adebayor pale mbele.

Mechi hii ya leo ya ngao ya hisani itakuwa ni mechi ya tano ya Ngao ya Jamii kuchezwa nchini na ya pili kuishirikisha timu nje ya wapinzani wa jadi wa soka ya Tanzania, Simba na Yanga.

Mtibwa ilicheza na Yanga mwaka 2009, baada ya Simba kugoma na ikashinda mabao 2-1 na kutwaa Ngao, wakati kabla ya hapo, mwaka 2001, Ligi Kuu ya Tanzania ikiwa bado inadhaminiwa na Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), kupitia bia ya Safari Lager, ilichezwa mechi ya kwanza ya Ngao kihistoria.

Katika mechi hiyo, Yanga ilishinda mabao 2-1 dhidi ya Simba na mwaka juzi Yanga iliifunga tena Simba kwa penali 3-1 kufuatia sare ya 0-0 na mwaka jana, Simba ilitwaa Ngao ya kwanza katika historia yake, kwa kuifunga Yanga mabao 2-0.

Ikumbukwe mara ya mwisho Simba SC ilipokutana na Azam FC, katika Robo Fainali ya Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati, Kombe la Kagame, Julai mwaka huu, Dar es Salaam, ilifungwa mabao 3-1, yote yakifungwa na Bocco na lile la kufutia machozi kwa wekundu hao Msimbazi liliwekwa kimiani na kiraka Shomari Kapombe.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents