Michezo

Sio kwa Okwi huyu

Ligi kuu soka Tanzania Bara iliendelea tena hapo jana lakini macho na maskio ya wadau na wapenzi wasoka yalikuwa yameelekezwa huko katika Uwanja wa Uhuru ambapo mabingwa wa FA, Simba SC wakiwa wenyeji waliwakaribisha Mtibwa Sugar.

Katika mchezo huo ambao ulikuwa nakasi na vuta nikuvute baina ya timu zote mbili wenyeji wa mchezo huo Simba walikubali kuruhusu bao la mapema katika kipindi cha kwanza dakika ya 37 likifungwa na nahodha wa Mtibwa Sugar, Stamili Mbonde kwa njia ya kichwa.

Hadi dakika 90 za mchezo Mtibwa Sugar ilikuwa ikiongoza hali iliyopelekea hadi baadhi ya mashabiki wa Simba kukata tamaa na kuanza kuondoka Uwanjani.

Katika dakika tatu za nyongeza mshambuliaji wa timu ya taifa ya Uganda na klabu ya Simba, Emmanuel Arnold Okwi akaendeleza ufalme wake wa mabao baada ya kufunga goli lake la saba kwenye uwanja huo wa Uhuru na kuinusuru timu yake kupoteza kwa mara ya kwanza mechi ya ligi kuu msimu huu.

Bao safi la Emmanuel Okwi lilipatikana baada ya kupiga faulo iliyokwenda moja kwa moja kimyani ikiwa ni adhabu iliyotolewa na muamuzi baada ya mchezaji wa Simba, Erasto Nyoni kufanyiwa rafu karibu na kidimba cha penati.

Baada ya kumalizika kwa mchezo huo Emmanuel Okwi amesema “Mtibwa ni timu kubwa na nzuri tulikuwa tumesha fungwa lakini tunashukuru kwa matokeo haya.” Okwi ameyasema hayo kupitia Azam Tv.

Emmanuel Okwi sasa anafikisha jumla ya mabao saba katika ligi kuu ya Vodacom Tanzania Bara msimu huu akiwa ameingia dimbani mara tano wakati akifanikiwa kufunga mabao yote katika michezo ya Dar es salaam.

Kwa matokeo ya hapo jana Okwi ameiwezesha Simba kurejea tena kileleni mwa ligi kwa kuwa na jumla ya pointi 12 sawa na watani zao wa jadi klabu ya Young Africans, Azam FC na Mtibwa Sugar lakini wakiwa na tofauti nzuri ya magoli.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents