Sitta atishia kushtaki magazeti

Spika Samuel SittaBAADA ya kutangaza kumwagiza Katibu wa Bunge kuandaa taarifa za mapato na matumizi yake tangu aingie bungeni ikiwa ni njia ya kujibu tuhuma mbalimbali dhidi yake, Spika wa Bunge, Bw. Samuel Sitta sasa anaonekana kuchukua hatua nyingine kali zaidi

Na Mwandishi Wa Majira




BAADA ya kutangaza bungeni hivi karibuni kuwa amemwagiza Katibu wa Bunge kuandaa taarifa za mapato na matumizi yake tangu aingie bungeni ikiwa ni njia ya kujibu tuhuma mbalimbali dhidi yake, Spika wa Bunge, Bw. Samuel Sitta sasa anaonekana kuchukua hatua nyingine kali zaidi ya kujisafisha kwa kutishia kwenda kortini.

Hatua hiyo imebainika baada ya uchunguzi wa gazeti hili kubaini kuwa Spika Sitta amewaagiza wanasheria wake kuyaandikia barua baadhi ya magazeti na kuyaarifu juu ya nia yake ya kwenda mahakamani iwapo hayatamwomba radhi kwa tuhuma mbalimbali walizoziandika kumhusu yeye.

Kwa mujibu wa barua ya mawakili wa kampuni ya Esco Law Chambers ya jijini Dar es Salaam ambayo pia Bw. Sitta ni mmoja wa wamiliki waendeshaji, Spika ameanza kwa kulitaka gazeti moja la kila wiki linaloandika habari za kijamii na mikasa limwombe radhi katika kipindi cha siku saba la sivyo atachukua hatua za kisheria.

“Bw. Sitta kwa nguvu zote anakana tuhuma mlizoziandika na ametuagiza kwamba…mchapishe matoleo matatu yanayofuatana ya taarifa za kukanusha mliyoyaandika,” ilisema barua ya mawakili hao yenye kumbukumbu namba ESCO/Gen/08/17 ya April 14 mwaka huu.

Barua hiyo iliyosainiwa na wakili Paul Kihwelo inaonesha kuwa miongoni mwa mambo yaliyomkera Spika na kuona kuwa ameshushiwa hadhi yake ni pamoja na habari iliyoandikwa na gazeti hilo inayohusu matumizi juu ya matibabu yake na duka analodaiwa kununua dawa hizo.

“Msipotekeleza matakwa hayo katika kipindi cha siku saba, tuna maagizo ya dhati kabisa ya kuwachukulia hatua za kisheria kwa kufungua kesi katika mahakama za kisheria bila kuwaarifu tena na mtawajibika kwa gharama zote zitokanazo…Kwa sasa tunawashauri mfanye kazi zenu kwa mujibu wa sheria,” imehitimisha barua hiyo.

Hata hivyo tofauti na wanasiasa wengine, Spika katika barua yake hiyo hakutaka gazeti hilo limlipe fidia yoyote ya fedha zaidi ya ombi la kuwataka wakanushe habari yao kwenye ukurasa wa mbele.

Hivi karibuni taarifa ya ofisi ya Bunge ilieleza kuwa tangu Bunge lilipopitisha mapendekezo juu ya hatua kali zinazopaswa kuchukuliwa dhidi ya wote waliohusika katika kashfa ya Richmond, kumekuwa na dalili za baadhi ya watu wenye malengo binafsi kumsumbua Spika Sitta.

Taarifa kadhaa zinazojaribu kumchafua kiongozi huyo zimekuwa zikisambazwa kupitia mtandao wa intaneti, lakini akihutubia mwanzoni mwa kikao cha 11 cha Bunge kinachoendelea mjini Dodoma Spika Sitta aliziita siasa za namna hiyo kuwa ni za “maji taka,” na kusisitiza kuwa haziwezi kumsumbua, atapambana nazo.

Iwapo atakwenda mahakamani, atakuwa kiongozi wa kwanza wa Bunge kuchukua hatua hiyo dhidi ya vyombo vya habari nchini.

Wakati akichukua hatua hiyo, Mwandishi Reuben Kagaruki anaripoti kuwa baadhi ya wanasiasa wameshauri iundwe tume maalum itakayochunguza tuhuma hizo zilizoibuliwa dhidi ya Bw. Sitta.

Mbali na hiyo wameshauri hesabu za matumizi ya fedha ndani ya Bunge na Baraza la Wawakilishi ziwe zinafanywa na wakaguzi huru kwa lengo la kuweka mambo wazi au kiundwe chombo maalum cha kuchunguza tuhuma zinazohusiana na ufisadi kwa kuwa wananchi hawana imani tena na Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (TAKUKURU).

Wanasiasa hao walitoa kauli hizo kwa nyakati tofauti Dar es Salaam jana walipozungumza na gazeti hili kuhusiana na tuhuma zilizosambazwa kwenye mtandao wa inteneti zikieleza kuwa Spika Sitta amelipwa sh. milioni mbili katika kipindi cha wiki mbili kwa ajili ya kununua dawa.

Mbali na hiyo imeripotiwa kuwa Bw.Sitta amekuwa akilipwa kiasi kikubwa cha fedha katika safari anazofanya ndani na nje ya nchi na kwamba amejilimbikizia deni kubwa linalotajwa kufikia sh. milioni 60.

Licha ya Bw. Sitta kutupilia mbali tuhuma hizo na kuagiza Katibu wa Bunge kuandaa hesabu za matumizi yake, wanasiasa waliozungumza na Majira walisema haiwezekani mtu akajitibia kisha kujichunguza ili kujua kama amepona.

Mwenyekiti wa Tanzania Labour Party (TLP), Bw. Augustino Mrema, alisema Bw. Sitta anapaswa kuundiwa tume ili kubaini ukweli.

“Tunataka iundwe tume sio yeye kutuletea mahesabu zake sisi si watoto wadogo,” alisisitiza Bw. Mrema. Alisema hata kama Bw. Sitta alifanya kazi tangu enzi za Marehemu Mwalimu Julius Nyerere, na kujivunia kufuata maadili hiyo haitoshi kwa sababu tangu ‘aondoke’ (Nyerere) watu wanajifanyia wanavyotaka.

Alisema ikibidi tume itakayoundwa kumchunguza Bw. Sitta itoke miongoni mwa wabunge kwani wameonesha kuwa wapo wenye uwezo wa kufanyakazi hiyo vizuri. “Spika asije kutupa hesabu za ‘magreen'(bandia) tunachohitaji ni tume ya kuchunguza jambo hili,” alisisitiza Bw. Mrema.

Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa CUF, Bw. Juma Duni Haji alisema ingawa huwa hapendi kuzungumzia mambo yanayohusu Bunge lakini kwa sakata linalomgusa Spika Sitta ana imani hawezi kujitibia na kisha kujichunguza. Alisema wakati umefika sasa hesabu za Bunge ziwe zinafanywa na mkaguzi kama inavyofanyika kwenye mabenki.

“Mimi sifahamu ni kwa nini mkaguzi haendi hata kwenye Bunge na Baraza la Wawakilishi,” alihoji Bw. Duni na kuongeza kuwa kama mkaguzi anafanya ukaguzi hadi Mahakama Kuu haoni sababu ya hilo kushindikana hata kwa Bunge.

Alisema amekuwa akimsikia Spika wa Baraza la Wawakilishi akisema wawakilishi wa CUF wamekatwa posho kwa kususia vikao lakini hakuna anayejua kinachoendelea baada ya hapo. Walisema wanaotakiwa ni wakaguzi huru wa kufanya kazi hiyo.

Katibu Mkuu wa CHADEMA, Dkt. Willbroad Slaa, alisema si busara kila jambo kuundiwa tume lakini akashauri kuwepo chombo maalum cha kushughulikia tuhuma za aina hiyo. Alisema kwa sasa watu wameishapoteza imani na TAKUKURU hivyo chombo cha aina hiyo kinahitajika.

Alitoa mfano akisema kuwa hata yeye ametuhumiwa kula fedha za walemavu ili ukweli uweze kujukana nilazima kuwepo na chombo cha kuwachunguza madai hayo na si TAKUKURU.

Kuhusu agizo la Spika kuagiza Ofisa ya Bunge kuandaa hesabu za matumizi yake, Dkt. Slaa alisema hilo ni jambo zuri ili watu wanaotaka kuhoji wajue pa kuanzia.

Wakati sakata hilo linazidi kufukuta tayari Katibu wa Bunge, Bw. Damian Foka, amekaririwa na vyombo vya habari akisema kuwa ofisi za Bunge hazina taarifa za Spika kughushi risti badala yake alipendekeza apewe muda ili atafute ukweli

Bw. Foka alikiri madai yaliyoandikwa kwenye mtandao intaneti kuwa Bw. Sitta aliwasilisha risiti ya sh. milioni mbili aliyonunulia dawa kutoka duka moja lililopo Oysterbay, Dar es Salaam.

Pia alikiri kuwa Februari mwaka huu alilipwa sh. milioni mbili katika kipindi cha wiki moja kwa ajili ya kununulia dawa katika duka la Oysterbay. Kuhusu madai kuwa Spika amekuwa akilipwa fedha nyingi katika safari zake ndani na nje na kwamba amejilimbikizia deni la sh. milioni 60, Bw. Foka alisema huwa analipiwa huduma ya maradhi na nusu ya asilimia 20 ya posho kama fedha za matumizi na si zaidi ya hapo.


 


Source: Majira

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents