Habari

Sitta: Sina ushahidi dhidi ya Chitalilo

SPIKA wa Bunge, Samuel Sitta, amesema ofisi yake haijapokea barua toka ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai, inayoeleza kwamba Jeshi la Polisi limethibitisha kwamba Mbunge wa Buchosa, Samwel Chitalilo, alighushi cheti cha elimu ya sekondari kwamba alisoma katika shule moja iliyopo nchini Uganda.



na Happiness Katabazi


SPIKA wa Bunge, Samuel Sitta, amesema ofisi yake haijapokea barua toka ofisi ya Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai, inayoeleza kwamba Jeshi la Polisi limethibitisha kwamba Mbunge wa Buchosa, Samwel Chitalilo, alighushi cheti cha elimu ya sekondari kwamba alisoma katika shule moja iliyopo nchini Uganda.



Akizungumza kwenye mahojiano maalumu na Tanzania Daima nyumbani kwake jijini Dar es Salaam mapema wiki hii, Spika Sitta alisema ofisi yake imekuwa ikisikia mitaani kwamba Jeshi la Polisi lilifanya upelelezi na kubaini kwamba mbunge huyo ameghushi vyeti.



“Ujue ofisi yangu inasikia habari hizo mitaani tu, lakini taarifa hizo hazijafika ofisini kwangu kwa barua, hivyo siwezi kutolea uamuzi suala hilo na kwa mujibu wa sheria za nchi hii, polisi inapojiridhisha kwamba raia au kiongozi fulani amefanya kosa, wanampeleka mahakamani na hatimaye mahakama ndiyo chombo pekee kinathibitisha iwapo mtu huyo ana hatia au la.



“Lakini siyo polisi imethibitisha, basi ndiyo mtu ana hatia, hapana, sheria haisemi hivyo, ni lazima apelekwe mahakamani ithibitike. Ni mara ngapi polisi inasema ina ushahidi wa labda mtuhumiwa fulani, lakini wakimfikisha mahakamani na ushahidi wao, mahakama inamwachilia huru mtuhumiwa huyo? Nashauri sheria zifuatwe,” alisema Spika Sitta.



Alipotakiwa kuelezea tuhuma kuwa wabunge wengi awamu hii wameghushi vyeti vyao, Sitta alisema kuwa tuhuma hizo zitaendelea kuwa tuhuma, na wabunge hao kuonekana kuwa hawana hatia, hadi hapo itakapothibitishwa na mamlaka husika.



Alisema kwa sasa kuna uhuru mpana wa vyombo vya habari wa kusema lolote tofauti na miaka ya nyuma, na asingependa wabunge wahukumiwe kutokana na tuhuma, kwani watu wanaweza kuvitumia vyombo vya habari kuwachafulia wenzao.



Aliwataka wananchi watambue kuwa, chaguzi za sasa zina ushindani mkali, na wagombea wapo tayari kutumia mbinu zozote kuhakikisha kuwa wanashinda.



“Wakati mwingine watu huandaa kashfa kwa mbunge aliyepo madarakani, kama mbinu ya kumchafulia ili watakapogombea katika uchaguzi mwingine, amshinde kirahisi.



“Kwa sababu hizo, napenda wabunge wahukumiwe kwa yale yaliyothibitika, siyo kwa tuhuma. Ofisi yangu kila kukicha inapokea barua nyingi sana kuhusu tuhuma za baadhi ya wabunge, na baadhi ya tuhuma tumekuwa tukizipeleka polisi, ili wazichunguze, lakini polisi wakishachunguza wanatuambia tuhuma hizo hazina ukweli wowote.



“Tuhuma nyingine zinazoletwa pale ofisini kwangu, nikikuelezea unaweza kucheka, utakuta mtu alishindwa kura za maoni, anatumia makundi yake kumchafua mbunge aliyepo madarakani, mfano mmoja kuna barua ilikuja pale ofisini, mtu huyo kaniandikia nimchunguze mbunge fulani kwamba wakati alipokuwa motto, aliwahi kuiba baiskeli kijijini, sasa tuhuma kama hizi ni za kijinga,” alisema Spika Sitta.



Februari mwaka huu, Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), Robert Manumba, aliliambia gazeti hili kwa njia ya simu, kwamba polisi ilifanya uchunguzi kuhusu tuhuma za kughushi cheti, zinazomkabili Chitalilo na kuthibitisha kuwa ni kweli Chitalilo alighushi cheti.



Hata hivyo, tangu kutolewa kwa kauli hiyo, hakuna hatua zozote zilizochukuliwa dhidi ya mbunge huyo ambaye anaendelea na kazi zake na zile za kisiasa kama kawaida hali ambayo imekuwa ikilalamikiwa na Watanzania wengi kuwa Jeshi la Polisi linaogopa kumchukulia hatua Chitalilo kwa sababu ni mbunge wa chama tawala – CCM.


Source: Tanzania Daima

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents