Habari

Soko la Moshi laungua

Moto mkubwa umelipuka katika Soko Kuu la mjini Moshi na kusababisha hasara ya Sh. milioni 300 za Kampuni ya simu ya Vodacom mkoani Kilimanjaro.

Na Jackson Kimambo, PST, Moshi

 

Moto mkubwa umelipuka katika Soko Kuu la mjini Moshi na kusababisha hasara ya Sh. milioni 300 za Kampuni ya simu ya Vodacom mkoani Kilimanjaro.

 

Moto huo pia umetekeza zaidi ya vibanda 50 vya biashara vilivyokuwa vimezunguka nje na ndani ya soko hilo.

 

Aidha, zaidi ya wafanyabiashara 280 wameathirika na moto huo baada ya bidhaa zao kuteketezwa.

 

Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Bw. Lucas Ng`ohoboko alisema kuwa moto huo ulizuka sokoni hapo saa saba za usiku wa Machi 24 na kusababisha hasara ya mamilioni ya fedha ya wafanyabiashara wa soko hilo.

 

Hata hivyo, hakuna mtu aliyekufa na ulifanikiwa kuzimwa baada ya jitihada zilizofanywa na magari ya zimamoto ya kiwanda cha Sukari cha TPC na la Uwanja wa Ndege wa kimataifa wa Kilimanjaro (KIA).

 

Kamanda Ng’ohoboko alisema, polisi walitoa taarifa za moto huo kwa Halmashauri ya Manispaa ya Moshi lakini gari lilipofika lilikuwa halina maji ya kuzima moto huo.

 

Alisema kuwa pamoja na magari hayo kununuliwa hivi karibuni, hayaweki maji ya tahadhari ikiwa ni pamoja na koki zake kugoma kufunguka wakati wa harakati za kuzima moto huo.

 

Akiongea na waandishi wa habari, Meneja wa kanda wa kampuni ya Vodacom mjini hapa, Bw. Jackson Kiswaga, alisema kuwa moto huo umeisababishia kampuni hiyo hasara ya Sh. milioni 300 kutokana na vifaa vilivyoteketea kwa moto huo.

 

Bw. Kiswaga alivitaja baadhi ya vifaa hivyo kuwa ni Signal Genereta yenye thamani ya Sh. milioni 40 na kifaa cha kupimia ubora wa sauti (PCM Analyeser) chenye thamani ya Sh. milioni 20.

 

Mmoja wa wafanyabiashara aliyeathirika na moto huo, Bw. Emmanuel Mlay, alisema kuwa janga la moto huo limemsababishia hasara kubwa na umekuja kipindi ambacho alikuwa amejiwekea malengo ya kuhakikisha kwamba anaiboresha biashara yake na tayari alishakuwa ameongeza mtaji wa kutosha kwa kununua mali kwa wingi.

 

`Hili ni pigo kwangu, kwa familia yangu na kwa wafanyabiashara wenzangu� Hatujui hatima yetu kwani wengi kati yetu tulikuwa tumechukua mikopo kutoka katika taasisi mbali mbali za kifedha,` alilalamika kwa uchungu Bi.Swaumu Kiramo.

 

Chanzo cha moto huo bado hakijajulikana na Kamanda wa Polisi mkoani hapa, Bw. Ng’ohoboko, alisema kuwa upelelezi kuhusu tukio hilo unaendelea.

 

Wakati huo huo, katika eneo la Boma Mbuzi, Kata ya Pasua mjini hapa Nyumba ya Diwani wa CHADEMA, Bw. Jaffery Michael imeteketea kwa moto na kusababisha pikipiki mpya 50 kuteketea kwa moto na nyingine 90 zikiwa zimeharibika vibaya baada ya kuokolewa na wasamalia wema.

 

Kamanda Ng`ohoboko alisema tukio lilitokea Machi 23, saa tisa za mchana ambapo pia moto huo uliteketeza jenereta mbili aina ya Honda ambapo alisema nyumba hiyo alikuwa anaishi diwani huyo na familia yake wakati upande wa pili wa nyumba hiyo ulikuwa ukitumika kama stoo ya kuhifadhi vitu.

 

Kwa mujibu wa Kamanda Ng’ohoboko, hasara ya vitu vilivyoteketea na moto huo haijajulikana na kwamba hakuna mtu yeyote aliyepoteza maisha wala kujeruhiwa.

 

Source: Nipashe

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents