Spika amshangaa Zitto

SPIKA wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samuel Sitta, ameeleza kushangazwa kwake na kitendo cha Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto, kumuandikia barua akimtaka aiagize Kamati ya Kanuni ya Bunge kupitia upya adhabu aliyopewa.

na Tamali Vullu


SPIKA wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samuel Sitta, ameeleza kushangazwa kwake na kitendo cha Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Kabwe Zitto, kumuandikia barua akimtaka aiagize Kamati ya Kanuni ya Bunge kupitia upya adhabu aliyopewa.


Zitto alisimamishwa kuhudhuria vikao vya Bunge Agosti 14, mwaka huu, kwa madai ya kusema uongo wakati akiwasilisha hoja binafsi akitaka Bunge liunde kamati kuchunguza, pamoja na mambo mengine, kusainiwa kwa mkataba wa mradi wa mgodi wa Buzwagi nje ya nchi.


Mkataba huo ulisainiwa na Waziri wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi mapema mwaka huu katika hoteli moja jijini London, Uingereza.


Akizungumza na Tanzania Daima jana kwa njia ya simu, Sitta, alisema ingawa bado hajapata barua hiyo, lakini amezisoma habari kuhusu hatua ya Zitto katika vyombo vya habari.


Alisema kuwa baada ya kusoma, hakutegemea barua ya aina hiyo inaweza kuandikwa na Mbunge wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.


“Bado sijapata barua, ndiyo kwanza narejea kutoka India, lakini sikutegemea mbunge katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anaweza kuandika barua ya aina hiyo, ingawa kila mtu ana uhuru wa kuzungumza.


“Barua hiyo nimeisikia kwenye vyombo ya habari, ina maneno ya ajabu, nasubiri nipate barua hiyo ndiyo nitajua la kufanya,” alisema Spika.


Katika barua hiyo, Zitto analitaka Bunge kupitia Kamati ya Kanuni, lipite adhabu hiyo kwa kuwa anaamini kuwa haikuwa ya haki, imemuonea na kumdhalilisha mbele ya macho ya jamii ya Kitanzania na kimataifa.


Anaainisha maombi sita, akiamini kuwa kupitia hatua anazoliomba Bunge kuzipitia, ametoa nafasi kwa mhimili huo wa utawala kujikosoa, kujisahihisha na kujirekebisha kutokana na makosa liliyoyafanya kwa kumuadhibu pasipo kuzingatia kanuni.


Ingawa Zitto ameahidi kuyaheshimu maamuzi yatakayofikiwa iwapo hatua hizo zitafuatwa, lakini iwapo atabaini kuwa haki haikutendeka, anaweza kuchukua hatua ya kulifikisha suala hilo mahakamani, ili kuhakikisha anatetea haki yake.


Katika maombi yake sita, Zitto analiomba Bunge, kupitia Kamati ya Kanuni za Bunge, kupitia adhabu aliyopewa Agosti 14, mwaka huu na lijiridhishe kama kanuni za Bunge zilifuatwa.


Aidha, baada ya kupitia vifungu vyote na kumsikiliza yeye katika kikao cha kamati, Zitto analitaka Bunge lipitie kauli za viongozi wote wa Bunge na serikali kuhusu adhabu aliyopewa na kuona kama hawakuvunja kanuni za Bunge na sheria namba 3 ya mwaka 1988.Pia, anataka iwapo itabainika kuwa kulikuwa na makosa katika kumuadhibu, basi Bunge limuombe radhi kwa kumpa adhabu isivyo halali.


Aidha, analitaka Bunge lijutie maamuzi liliyoyachukua na kuahidi mbele ya jamii kuwa, halitarudia kuvunja kanuni za Bunge kwa makusudi na kumuadhibu mwakilishi wa wananchi mwingine bila makosa.


Akihojiwa juzi ni kwa nini anaamini kuwa adhabu hiyo haikuwa ya haki, Zitto alisema hatua za kumuadhibu hazikufuata kanuni za Bunge, hazikuzingatia tamaduni za Bunge na kubwa zaidi hazikumpa nafasi ya yeye kujitetea.


Zitto alibainisha katika barua hiyo kuwa, Bunge lina taratibu za kuleta hoja bungeni ambazo zimefafanuliwa kinagaubaga katika kanuni ambazo zinaanisha wazi kabisa kuwa hoja haiwezi kutolewa juu ya hoja nyingine, na kwamba muda wa kutoa taarifa ya hoja umewekewa utaratibu ndani ya kanuni za Bunge.


“Kanuni zetu zinasema wazi kabisa (59-3) kuwa iwapo mbunge anashutumiwa kusema uongo bungeni, au kutoa lugha ya kuudhi, atapewa muda ili kuthibitisha hili analoshutumiwa.


“Mimi Mheshimiwa Spika, si tu sikuwahi kushutumiwa kusema uongo, bali pia wewe binafsi unajua sijawahi kupewa muda kuthibitisha chochote,” anasema Zitto.


Anaongeza kuwa, alisimamishwa kwa kusema uongo bungeni, lakini hajaelezwa mahala popote uongo huo ni upi.


Zitto anabainisha katika barua hiyo kuwa mbaya zaidi baadhi ya viongozi wa Bunge akiwamo Spika, Naibu wake na Katibu wa Bunge, waliendelea kuonyesha kuwa adhabu aliyopewa ilikuwa sahihi na kuwaaminisha wananchi kuwa yeye ni muongo.


“Vile vile viongozi wa upande wa serikali, akiwemo waziri mkuu, mawaziri na manaibu mawaziri wamenukuliwa na vyombo vya habari wakisema mimi ni muongo kufuatia adhabu hiyo,” anasema.


Anasema kuwa licha ya kumdhalilisha yeye kama mtu binafsi, adhabu hiyo ni ishara mbaya sana kwa demokrasia ndani ya Bunge.


Zitto alisema angependa kuona Bunge likiheshimika na ndiyo maana akaamua kuitumikia adhabu yote na kutotoa kauli yoyote iliyoingilia mamlaka ya Bunge kuhusiana na adhabu hiyo.


“Mheshimiwa Spika, ombi langu hili mbele yako ni muhimu sana katika kulifanya Bunge lijiangalie na kujirekebisha, kama inabidi, pale ambapo litakuwa limekosea. Hii itasaidia kuepuka makosa kama haya siku za usoni,” anasema Zitto katika barua hiyo.


Zitto, alisimamishwa kuhudhuria vikao vya Bunge kutokana na hoja iliyotolewa na Mbunge wa Mchinga, Mudhihir Mudhihir, akidai kuwa mbunge huyo alikuwa amelidanganya Bunge katika hoja yake binafsi aliyoiwasilisha awali.


Katika hoja hiyo binafsi, Zitto alikuwa analitaka Bunge liunde kamati teule kuchunguza hatua ya Waziri Karamagi, kusaini mkataba wa mradi wa mgodi wa Buzwagi nje ya nchi.


Hoja hiyo iliungwa mkono na wabunge wengi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ambao siku hiyo hiyo walipitisha azimio la kumsimamisha mbunge huyo.


Source: Tanzania Daima

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents