Jiunge ufaidi miezi 2 bure!

SUMATRA watoa kauli kuhusu tiketi zilizoandikwa ‘Mke mmoja analemaza akili’

Kwa watu wanaopanda magari ya Mbagala-Kivukoni jijini Dar es salaam kumekuwa na tiketi za baadhi ya mabasi zikiwa zimeandikwa ujumbe unaosomeka ‘Mke mmoja analemaza akili’, Ujumbe ambao umeonekana kuwakera baadhi ya watu na kupelekea picha za tiketi hizo kusambaa kwa kasi kwenye magroup ya WhatsApp wengi wakidai kuwa ujumbe huo upo kinyume na maadili, hatimaye SUMATRA wametoa neno.

Mamlaka hiyo ya Udhibiti wa Usafiri wa Majini na Nchi Kavu, imetoa ufafanuzi kuhusu tiketi hizo na kusema kuwa hakuna adhabu ya moja kwa moja kwa mabasi yenye tiketi zenye ujumbe kama huo au ujumbe wenye kiashiria cha kuvunja maadili lakini gari husika linaweza kuadhibiwa kwa makosa mengine kama kushindwa kufuata taratibu.

Hakuna adhabu ya moja kwa moja kwa gari lenye tiketi yenye ujumbe usiokuwa na maadili, lakini gari husika linaweza kuadhibiwa kwa kosa la kushindwa kufuata taratibu, sheria za barabarani, pamoja na sheria zinginezo, ambayo faini yake ni Sh. 250,000,” amesema Meneja Leseni wa Sumatra, Leo Ngowi kwenye mahojiano yake na gazeti la Nipashe.

Akifafanua vifungu vya sheria za SUMATRA kuhusu tiketi, Ngowi amesema kwa mujibu wa kanuni za Sumatra, kifungu namba 33(2) (a) inayohusu mabasi yaendayo nje ya miji, tiketi zao zinapaswa kuwa na jina la abiria na namba ya kiti.

Pia, tiketi inapaswa kuonesha muda wa kuwasili na kuondoka kituoni, kituo cha kuondokea, pamoja na njia itakayopita na mwisho wa safari.

Kwa mabasi/daladala zinazofanya safari za ndani, tiketi zinapaswa kuwa na namba ya usajili ya gari, njia ya gari itakayopitia, nauli halisi, tarehe ya kukata tiketi, pamoja na namba ya leseni.

Kwa upande mwingine, Sumatra imewataka abiria watakapopewa tiketi zenye ujumbe unaoshabihiana na huo, watoe taarifa kwenye mamlaka hiyo kwa kuandika barua ya malalamiko pamoja na kuambatanisha tiketi husika.

Related Articles

Bongo5

FREE
VIEW