Habari

Taarifa kutoka jeshi la polisi mkoani Mbeya

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limeendelea kufanya misako, operesheni na doria zenye tija katika maeneo mbalimbali ili kudhibiti uhalifu na wahalifu na limekuwa likishirikiana na wananchi na wadau wengine katika jitihada hizo za kukabiliana na uhalifu na wahalifu na kupata mafanikio makubwa ikiwa ni pamoja na kupungua kwa matukio makubwa ya uhalifu.

Mafanikio yaliyopatikana katika Misako/Doria ni kama ifuatavyo:-

KUPATIKANA NA NOTI BANDIA.

Mnamo tarehe 22.10.2017 majira ya saa 15:00 Alasiri, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya lilifanya msako huko eneo la Sisimba lililopo Kata na Tarafa ya Sisimba, Jiji na Mkoa wa Mbeya na kufanikiwa kumkamata mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la FAUSTINA MAGANGA [20] Mkazi wa Mtaa wa Teku akiwa na noti bandia 10 za Tshs 10,000/= sawa na Tshs 200,000/= kama zingekuwa halali.

Noti hizo zilikuwa na namba BU 3352850 noti 5 na BU 3352846 noti 5. Mtuhumiwa atafikishwa Mahakamani mara baada ya upelelezi kukamilika.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linaongeza jitihada za kuzuia na kupunguza matukio ya ajali za barabarani kwa kuhakikisha madereva na watumiaji wengine wa barabara wanafuata sheria na alama za usalama Barabarani. Aidha kumekuwa na ajali 01 ya vifo na majeruhi kama ifuatavyo:-

Mnamo tarehe 22.10.2017 majira ya saa 15:45 jioni huko maeneo ya DM Hotel, Kata ya Bulyaga, Tarafa ya Tukuyu mjini, Wilaya ya Rungwe, Mkoa wa Mbeya katika Barabara kuu ya Tukuyu/Mbeya, Gari yenye namba za usajili T 756 BGS aina ya Toyota Chaser iliyokua ikiendeshwa na dereva aitwaye CHARLES MWAMBENA [26] Mkazi wa Tukuyu ikitokea Kitongoji cha Bagamoyo kuelekea Tukuyu mjini iliacha njia na kwenda kuwagonga watembea kwa miguu wawili 1. BENARD FORTNATUS KASELA [22] Mwanachuo wa FDC – Katumba na Mkazi wa Nansio – Ukerewe na 2. AYOUB WILLIAM MWAIJENGO [20] Mwanachuo wa FDC – Katumba, Mkazi wa mbeya na kusababisha vifo vyao wakiwa wanapatiwa matibabu katika Hospitali ya Wilaya – Makandana.

Inadaiwa kuwa Gari hilo baada ya kuwagonga watembea kwa miguu lilipinduka na kisha kutumbukia mtaloni. Aidha katika ajali hiyo watu watatu walijeruhiwa akiwemo dereva wa Gari hilo na watu wengine wawili ambao walikuwa katika gari hilo ambao ni ALLAN JAMES ALLAN [30] Mkazi wa Bagamoyo na NKUNDWE JOEL KASOKELA [29] Mkazi wa Msasani.

Chanzo cha ajali kinachunguzwa. Majeruhi wamehamishiwa Hospitali ya Rufaa Mbeya kwa matibabu zaidi. Mtuhumiwa ambaye ni dereva wa gari hiyo amekamatwa na amelazwa Hospitali ya Wilaya ya Rungwe – Makandana akiwa chini ya ulinzi wa Polisi. Miili ya marehemu imehifadhiwa Hospitali ya Wilaya ya Rungwe – Makandana.

Aidha Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limeendelea kukabiliana na matukio makubwa ya uhalifu pamoja na wahalifu. Jitihada zinaendelea kwa kushirikiana na wananchi kuhakikisha Mkoa wetu unakuwa mahala salama. Hata hivyo Kumekuwa na matukio 02 ya mauaji kama ifuatavyo:-

Mnamo tarehe 22.10.2017 majira ya saa 13:00 mchana huko Kijijj cha Mwala, Kata ya Ilembo, Tarafa ya Isangati, Wilaya ya Mbeya Vijijini, Mkoa wa Mbeya, Mtu mmoja aliyefahamika kwa jina la ASA MWILE @ MWASENGA [21] Mkazi wa Kijiji cha Masoko aliuawa kwa kupigwa na kundi la wananchi walioamua kujichukulia sheria mkoanani wakitumia silaha za jadi fimbo na mawe.

Inadaiwa kuwa chanzo cha tukio hilo ni tuhuma za wizi baada ya marehemu kukutwa akivunja duka mali ya ZICKY YORAM [34] Mkazi wa Mwala hivyo wananchi kupiga yowe na kuanza kumshambulia hadi kufa. Mwili wa marehemu umehifadhiwa Hospitali Teule ya Ifisi. Upelelezi unaendelea

Mnamo tarehe 22.10.2017 majira ya saa 07:00 asubuhi huko maeneo ya Sai, Kata ya Ilomba, Tarafa ya Iyunga, Jiji na Mkoa wa Mbeya. Mtu asiyefahamika jina wala anuani yake mwenye jinsia ya kiume anayekadiriwa kuwa na umri wa miaka 20-30 jinsia ya kiume aliuawa kutokana na kupigwa na wananchi wanaojichukulia sheria mkononi.

Chanzo cha tukio ni tuhuma za wizi. Mwili wa marehemu umehifadhiwa Hospitali ya Rufaa Mbeya. Watuhumiwa wanne wamekamatwa kuhusiana na tukio hilo na mahojiano zaidi yanaendelea. Upelelezi unaendelea.

WITO:

Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Kamishina Msaidizi wa Polisi MUSSA A. TAIBU anatoa wito kwa Madereva kuwa makini wanapotumia vyombo ili kuepuka ajali zinazoweza kuepukika. Kaimu Kamanda TAIBU anawataka madereva kufuata, kuheshimu na kuzingatia sheria na alama za barabarani ili kuepuka ajali. Aidha anatoa wito kwa wananchi kuendelea kutoa ushirikiano kwa Jeshi la Polisi ikiwa ni pamoja na kutoa taarifa za uhali/wahalifu na watuhumiwa mbalimbali wa uhalifu ili wachukuliwe hatua stahiki za kisheria. Pia Kamanda TAIBU anawataka wananchi kutii sheria bila shuruti na kuacha kujichukulia sheria mkononi kwani ni kinyume cha sheria na kamwe Jeshi la Polisi halitakuwa na huruma na mtu yeyote wala kikundi cha watu watakaoshindwa kutii sheria.

Imesainiwa na:

[MUSSA A. TAIBU – ACP]

KAIMU KAMANDA WA POLISI MKOA WA MBEYA

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents