Habari

Taasisi za serikali zatakiwa kuweka kipaumbele ununuzi wa vifaa vya Maafisa habari

Watendaji wa Taasisi za Umma nchini zikiwemo Serikali Kuu na Mamlaka za Serikali za Mitaa na Tawala na Mikoa zimetakiwa kuweka kipaumbele katika kuwapatia vifaa vya kisasa Maafisa Habari, Mawasiliano na Uhusiano ili kuharakisha na kurahisisha mfumo wa utoaji wa habari na taarifa katika Taasisi zao.

Hayo yamesemwa Jijini Arusha na Waziri wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo Dkt. Harrison Mwakyembe wakati wa ufunguzi wa mkutano wa 14 wa kikao kazi cha Maafisa Mawasiliano Serikalini, kilichoanza tarehe 12-16 Machi, 2018.

“Serikali inaitambua na kuiheshimu kada hii muhimu ya mawasiliano ambayo ndiyo inayotoa taarifa za utekelezaji wa shughuli mbalimbali za Serikali kwa Wananchi, na hivyo ni wajibu wa watendaji wakuu wa taasisi za umma kuwawezesha,”alisema Dkt. Mwakyembe.

Dkt. Mwakyembe amesema kutokana na umuhimu huo, Taasisi za Serikali hazina budi kutoa kipaumbele katika ununuzi wa vifaa kwa Maafisa hao ili waweze kutoa taarifa za shughuli zinazotekelezwa ndani ya Taasisi zao pamoja na mipango ya Taasisi hizo kwa Wananchi wanaowaongoza.

“Utoaji wa habari kwa Wananchi sio utashi tena bali ni sheria inayosisitiza hilo. Serikali inatarajia Maafisa Habari kuwa wabunifu na kuhakikisha Wananchi wanapata haki yao ya kupata taarifa kuhusu Serikali yao,” alifafanua Dkt. Mwakyembe.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Habari Utamaduni Sanaa na Michezo, Susan Mlawi amesema Ofisi yake inatambua ndiyo msimamizi mkuu wa sekta ya habari hivyo wapo mstari wa mbele katika kuhakikisha kuwa Maafisa Habari wanajengewa uwezo wa kuisemea Serikali kwa kutoa taarifa sahihi na kwa wakati.

Kwa upande wake, Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Arusha Gabriel Daqqaro amesema Maafisa Habari wanategemewa Zaidi katika kuisaidia Serikali katika kutangaza kazi zinazofanywa na Serikali.

Hata hivyo, Mkurugenzi wa Idara ya Habari (MAELEZO) na Msemaji Mkuu wa Serikali wa Serikali ,Dkt. Hassan Abbasi amesema baada ya mkutano huo Maafisa Habari wa Taasisi, Idara za Serikali, Wizara, Mikoa, Majiji, Miji na Halmashauri zote nchini wataenenda kimkakati katika kutoa taarifa za Taasisi zao kwa Wananchi.

Kikao kazi cha Maafisa Mawasiliano Serikalini hufanyika kila mwaka kwa ushirikiano wa Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo pamoja na Chama cha Maafisa Mawasiliano Serikalini (TAGCO). Kikao hicho huusisha Maafisa Mawasiliano kutoka katika Taasisi, Idara na Wakala wa Serikali, Wizara, Mikoa, Majiji, Miji na Halmashauri zote Tanzania.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents