Siasa

Tabibu asema matumizi ya kondomu si halali

MGANGA wa zahanati ya Bigabilo iliyo chini ya Taasisi ya Dini ya Kikristo (FPCT) katika wilaya ya Kigoma mkoani hapa amesema matumizi ya kondomu si njia halali ya kutokomeza UKIMWI.

Na Jacob Ruvilo, Kigoma


MGANGA wa zahanati ya Bigabilo iliyo chini ya Taasisi ya Dini ya Kikristo (FPCT) katika wilaya ya Kigoma mkoani hapa amesema matumizi ya kondomu si njia halali ya kutokomeza UKIMWI.


Mganga huyo Bw. Emmanuel Geremia, alisema hayo wakati wa mafundisho kwa vijana wa dini hiyo ya kikristo katika Kanisa hilo la FPCT tawi la Bigabilo iliyofanyika juzi.


Alisema matangazo na vipeperushi vilivyotolewa kuwa mtu awe na mpenzi mmoja na kutumia kondomu si njia pekee ya kusaidia kuzuia UKIMWI.


Aidha, alisema katika semina walizojifunza yeye na wenzake imegundulika kuwa katika kila kondomu tano, moja huenda ikawa na vitundu ambavyo vinaweza kupitisha virusi vya UKIMWI na magonjwa mengine ya zinaa.


Mganga huyo ambaye pia ni kiongozi wa dini katika madhehebu hayo ya FPCT aliwataka vijana hao wapatao 20 waliohudhuria mafunzo hayo, kuwa njia pekee ya kutokomeza UKIMWI ni suala la kumwamini Mwenyezi Mungu kwa kufuata amri yake na kuachana na vitendo viovu.


Hata hivyo, Mganga huyo aliwashauri vijana hao kuwa tayari kwa nguvu zao zote kuumunga mkono Rais Jakaya Kikwete, katika kampeni zinazoendelea nchini za kupima na kujua afya zetu kama tumeathirika au la.


Akiwatahadharisha vijana hao waumini wa Kanisa hilo, Mganga huyo alisema kama hawatamwamini Mungu na kuachana na matumizi ya kondomu yasiyo na uhakika kwa asilimia fulani watajikuta wanatengwa na Kanisa kutokana na vitendo hivyo viovu.


Naye Mashaka Baltazar, anaripoti kutoka Musoma kwamba
mkoa wa Mara ni miongoni mwa mikoa inayoongoza kwa maambukizi mengi ya virusi vya UKIMWI nchini.


Kauli hiyo ilitolewa jana na Mkuu wa Mkoa huo, Luteni Kanali mstaafu Issa Machibya, wakati akizindua kampeni ya mkoa ya upimaji kwa hiari virusi vya UKIMWI, kwenye uwanja wa shule ya msingi Mukendo mjini humo.


Bw. Machibya alisema takwimu za watu waliojitolea damu mwaka jana, zlionesha kuwa asilimia 6.9 walionekana kuwa na maambukizi ya virusi vya UKIMWI.


Na katika vituo vya ushauri nasaha na kupima kwa hiyari mwaka huo maambukizi yalionesha kuwa asilimia 16.2, na kusema kuwa maambukizi hayo ni ya kiwango cha juu mno.


Source: Majira


 

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents