Tahadhari yatolewa kwa watu wanaotaka kusafiri wiki hii kwa njia ya maji
Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetoa tahadhari kwa wananchi na wanaotumia usafiri wa majini kufuatia kuwapo kwa upepo mkali katika mikoa ya Tanga, Lindi, Mtwara, Dar Es Salaam, Mwanza, Kigoma, Rukwa, Ruvuma, Geita, Simiyu, Mbeya, Njombe pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba.
Taarifa iliyotolewa jana usiku na kituo kikuu cha utabiri cha TMA imewataka watu wawe makini huku ikizitaka mamlaka zinazoshughulika na usafiri wa majini ziwe makini kwa kuchukua juu ya tahadhari hiyo kwa kuhakikisha hakuna maafa yanayoweza kutokea.
Chanzo cha upepo huo mkali unaotarajiwa kuvuma kwa siku nne katika Ukanda wa Pwani ya Bahari ya Hindi na maziwa yote makuu, Unatokana na kuimarika kwa hali ya hewa kwenye eneo la Kusini Mashariki mwa Bara la Afrika na mfumo wa upepo wa Kusini.