Michezo

Taifa Stars yapata udhamini wa bilioni 2.1

Shirikisho la Soka Tanzania TFF, limeingia mkataba mnono na kampuni ya Bia ya Serengeti {SBL} wenye thamani ya shilingi bilioni 2.1 ambao unaifanya SBL kuwa mdhamini mkuu wa Timu ya Taifa ya Tanzania (Taifa Stars).

Hii ni mara ya pili kwa kampuni hiyo ya Bia kuiunga mkono timu ya taifa baada ya kufanya hivyo kwa kipindi cha miakamitatu ilipo idhamini timu hiyo kati ya mwaka 2007 hadi 2011. Katika makubaliano hayo ambayo yamesainiwa leo na pande zote mbili,Taifa Stars itakuwa inapokea Shilingi milioni 700 kila mwaka kutoka SBL ambazo itakuwa ni pamoja na fursa za kuitangaza chapa ya SBL na soko lake wakati wa mechi za ndani na ugenini zitakazo chezwa na timu ya taifa.

Akizungumza wakati wa kusaini kwa mkataba huo, Mkurugenzi Mtendaji wa SBL,Helene Weesie alithibitisha uamuzi wa kampuni hiyo wa kuunga mkono sekta ya michezo nchini na kubainisha kwamba michezo sio tuinaburudisha bali pia inaunganisha mashabiki na pia ni chanzo cha kipato kwa vijana.

“Sisi SBL tunaona ni heshima kubwa kuidhamini timu yetu ya Taifa. Tumechukua hatua hii muhimu tukielewa kabisa mchango unaotolewa na sekta ya michezo katika maendeleo ya kiuchumi na kijamii. Tunaamini kwamba kuiunga mkono Taifa Stars sio tu kwamba
tunaendelea kukuza sekta ya michezo bali pia tunaimarisha soka la ndani, mchezo ambao Tanzania na Dunia kwa ujumla wanaupenda sana,” amesema Weesie.

Kwa upande wake, Rais wa shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania,Jamal Malinzi aliishukuru SBL kwa uungwaji mkono huo ambao alisema utasaidia sana katika kufanikisha maandalizi kwa upande wa timu na hata kuiletea ufanisi mzuri.

“Udhamini wa SBL umekuja kwa wakati muafaka,wakati ambapo timu yetu ya taifa ipo katika hatua za maandalizi kwa mashindano ya kikanda na kimataifa,” alisema Malinzi. Hafla ya kusainiwa kwa udhamini huo pia ilihudhuriwa na Waziri wa Habari,Utamadhuni na Sanaa na Michezo Dk Harrison Mwakyembe ambaye alitoa wito kwa makampuni mengine na watu wenye mapenzi mema kuiwezesha sekta ya michezo kupitia huduma zake za kijamii na programu za udhamini.

“Nimefurahi sana kualikwa hapa leo kushuhudia kusainiwa kwa makubaliano ya udhamini wa timu yetu ya Taifa Stars kati ya kampuni ya Bia ya Serengeti na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania {TFF}. Naishukuru sana Serengeti Breweries kwa kukubali kuwa mdhamini mkuu wa timu yetu ya Taifa Stars. Kitendo hiki kinadhihirisha kwa mara nyingine kwamba SBL haijihusishi tu na biashara bali pia ni mdau mkubwa katika jitihada za kuleta maendeleo ya michezo hapa nchini,” ameongeza.

“Aidha kama wizara inayohusika na michezo, na kwa kushirikiana na TFF, napenda kuihakikishia SBL na wapenzi wote wa Taifa Stars kwamba kiasi hiki cha fedha cha shilingi bilioni 2.1 kutoka SBL zitatumika ipasavyo ili kukuletea mabadiliko chanya katika maendeleo ya timu yetu ya mpira wa miguu,” amesisitiza.

“Naipongeza sana SBL kwa mchango wao mkubwa kwa maendeleo ya taifa letu na kwa njia ya kipekee, kwa kukubali kuidhamini timu ya Taifa Stars”,Napenda kuhakikishia SBL,TFF na wadau wengine ambao wako katika mstari wa mbele katika kukuza sekta ya michezo kwamba wizara yangu na hususan serikali ya awamu ya tano iko tayari kushirikiana nao ili kuharakisha kuleta mafanikio katika Nyanja hii muhimu katika maisha ya mtanzania.”
BY HAMZA FUMO

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents