Michezo

Taifa stars yarejea na dawa ya Lesotho

Timu ya Mpira wa Miguu ya Tanzania maarufu kwa jina la Taifa Stars, inatarajiwa kurejea leo kutoka Cairo nchini Misri, Stars inatarajiwa kutua Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere, jijini Dar es salaam saa 6.30 mchana.

Wachezaji wa timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’

Timu hiyo iliyosafiri kwa ndege ya Ethiopia, ilikuwa jijini Alexandria – Kaskazini kabisa mwa nchi ya Misri ambako ilipiga kambi ya wiki moja kujiandaa na mchezo dhidi ya Lesotho unaotarajiwa kufanyika Jumamosi Juni 10, mwaka huu kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Wachezaji wa timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ walivyokuwa katika mazoezi nchini Misri

Akizungumza mara baada ya mazoezi ya hapo jana, Kocha Mkuu wa Taifa Stars, Salum Mayanga amesema kimsingi amefanikiwa katika kile alichopangilia kukifanya akiwa Misri.

“Kwanza kabisa niweze kumshukuru Mungu. Tulisafiri salama na kufanya mazoezi kwa siku saba hapa Misri. Na leo jioni tunanza safari ya kuelekea Cairo kwa ajili ya safari ya kurudi nyumbani. Naam, kambi ilianza tarehe 23 mwezi uliopita pale Dar es Salaam na tukaja kuendelea huku Misri.

“Naweza kusema kuwa nimefanikiwa au tumefanikiwa. Kambi ni nzuri, mazingira ya kambi ni mazuri na tulifika mahali ambako hakuna mtu anayeweza kufanya mizunguko kutoka au kuingia kirahisi kwa sababu tulikuwa kwenye kambi ya Hoteli ya Nyota Tano, lakini ni Jeshi.

“Mazoezi ya kawaida ya kiufundi nayo tumefanya vema kwa maana tulipata vitu vyote tunavyovihitaji hasa katika mazoezi usiku kwa sababu mchezo wetu utakuwa usiku.Nawaomba tu Watanzania waje kuiunga mkono timu yao,” amesema Mayanga hapo jana.

Wachezaji wa timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ walivyokuwa katika mazoezi nchini Misri

Naye, Nahodha Msaidizi wa timu hiyo, Himid Mao Mkami, amesema kwamba kambi ilikuwa nzuri yenye mafanikio ambayo matunda yake yatakuja kuonekana katika michezo mbalimbali ya kimataifa ukiwamo wa Jumamosi dhidi ya Lesotho.

Mchezo huo dhidi ya Lesotho umepangwa kuanza saa 2.00 usiku ambako itakuwa ni mechi ya kwanza kwa Taifa Stars katika Kundi ‘L’ kuwania nafasi muhimu ya kucheza fainali za Kombe la Mataiafa ya Afrika (AFCON) za mwaka 2019 zitakazofanyika Cameroon.

Mbali ya Lesotho na Tanzania, mataifa mengine katika Kundi ‘L’ ni Uganda na Cape Verde ambao pia wikiendi ya Juni 9, 10 na 11, mwaka huu watakuwa katika mchezo wa kwanza pia kuwania nafasi hiyo

BY HAMZA FUMO

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents