Michezo

Taifa Stars Yashuka Dimbani Leo kuwakabili Burundi

Kilimanjaro Stars.
Timu ya taifa inayoiwakilisha Tanzania katika michuano ya Cecafa Tusker Challenge Cup “ Taifa Stars” leo inajitupa katika uwanja wa Nambole jijini Kampala kucheza mchezo wake wa pili wa kundi B dhidi ya timu ya Taifa ya Burundi “Int’hamba Murugamba”.
Mchezo huo utakaoanza majira ya saa 6 za mvchana, unatarajiwa kuwa mkali na wa kusisimua , kwani timu zote mbiili zinahitaji ushindi hasa hasa Taifa Stars baada ya timu ya Burundi kuanza kwa kishindo kwa kuifinga timu ya Somalia magoli matano kwa bila hivyo kuongoza kundi hilo kwa idadi hiyo ya magoli.
Naye kocha wa Kilimanjaro Stars, Mdenmark Kim Poulsen amesema kwamba uwezo wa timu yake unazidi kuimarika siku hadi siku na sasa ana matumaini ya kufanya vizuri zaidi katika michuano hii.
“Tuliweza kuwafunga Kenya (kwenye mchezo wa kirafiki jijini Mwanza), na jumapili tuliwafunga Sudan, timu zote nzuri, Sudan wapo juu yetu kiuwezo katika viwango vya FIFA. Kwangu siangalii sana viwango vya FIFA, mpira ni pale unapokuwa uwanjani,”alisema Poulsen.
Akilizungumzia kundi lake, B lenye timu za Sudan, Somalia na Burundi, alisema ni gumu na wanatakiwa kupambana ili kufika mbali.
Akiendelea, Poulsen amesema bado anawahitaji mno washambuliaji Mbwana Ally Samatta na Thomas Emanuel Ulimwengu wa TP Mazembe ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) , ambao hata hivyo wamezuiwa na klabu yao.
Kim alisema jitihada za kuwaomba Mazembe wawaruhusu wachezaji hao zinaendelea.
Tunamnukuu, “Sijui itakuwaje wasipokuja, itanibidi tu niwatumie wachezaji hawa hawa waliopo, najua nina mshambuliaji mmoja, lakini nitawatumia hawa hawa waliopo, Simon Msuva anaweza akawa mshambuliaji, nitafanyeje,”.
“Siwezi kuita mchezaji mwingine kutoka nyumbani kwa sasa, kwa sababu mtu lazima umuone uwezo wake, huwezi kumuita tu, kwa hivyo naomba Mungu tu Samatta na Ulimwengu waje,”alisema Kim.
Katika mchezo wa leo, Kim ambaye amekuwa akifuatilia kwa makini mashindano haya ili kujua uwezo wa timu zote, hatarajiwi kuwa na mabadiliko kwenye kikosi chake kutoka kile kilichoifunga Sudan 2-0.
Kama kawaida, Nahodha Juma Kaseja anatarajiwa kuanza, kulia akicheza Erasto Nyoni, kushoto Amir Maftah na mabeki wa kati, Kevin Yondan na Shomary Kapombe. Kiungo mkabaji Frank Domayo, wingi ya kulia Simon Msuva, kushoto Mrisho Ngassa kiungo mchezeshaji Salum Abubakar na Mwinyi Kazimoto atacheza nyuma ya mshambuliaji pekee, John Bocco ‘Adebayor’.
Mfumo wa sasa Kim unaonekana kuwa na tija kwa Stars, kwani analundika viungo wengi, huku akitumia mawinga ambao wanasababisha presha kubwa ya mashambulizi.
Leo kama Bocco atakuwa makini anaweza kufunga zaidi ya mabao mawili aliyofunga kwenye mchezo wa kwanza, kwani kama alivyosema timu inazidi kuimarika siku hadi siku.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents