Habari

Takukuru yachuja kampuni za kutafiti rushwa

TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) imeanza mchakato wa utafiti wa kisayansi ili kufahamu kiwango cha rushwa na ufisadi nchini na kurahisisha mapambano dhidi ya tatizo hilo.

Faraja Mgwabati



TAASISI ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) imeanza mchakato wa utafiti wa kisayansi ili kufahamu kiwango cha rushwa na ufisadi nchini na kurahisisha mapambano dhidi ya tatizo hilo.


Mkurugenzi Mkuu wa Takukuru, Edward Hosea, aliiambia HabariLeo jana kuwa utafiti huo utatoa taswira halisi ya hali ya rushwa zaidi ya ile inayotolewa na taasisi binafsi za ndani na nje ya nchi.


Tayari Taasisi ya kimataifa ya kupambana na rushwa na ufisadi duniani imetoa taarifa kwamba inatarajia kutangaza mwezi ujao matokeo ya utafiti wake wa hali ya rushwa duniani.


Hosea alisema ni vigumu kujua kama rushwa na ufisadi umepungua au umeongezeka kwa sababu hakuna taarifa sahihi za kisayansi za hali ya rushwa nchini na ndio maana taasisi hiyo imeamua kufanya utafiti huo.


Hosea alisema tayari Takukuru imetoa matangazo ya zabuni kwa kampuni yoyote ya ndani na nje kwa ajili ya kufanya utafiti huo na tayari wameanza kupokea maombi.


“Huu ni utafiti mkubwa wa kisayansi ambao haujawahi kufanyika nchini ambao utatusaidia sana kujua ukubwa wa tatizo la rushwa,” alisema Hosea.


Hata hivyo hakuweza kusema utafiti huo utagharimu kiasi gani na utachukua muda gani kwa maelezo kuwa
taarifa hizo zikiwekwa wazi zinaweza kuvuruga zoezi la kuchagua mshindi wa zabuni.


Akizungumzia kuhusu mapambano ya rushwa na ufisadi nchini alisema sheria ya mwaka 1971 ya kupambana na rushwa ilikuwa kikwazo kwa kuwa iligusa maeneo machache ya rushwa na mengine hayakuwa na ufafanuzi wa kutosha.


“Kuna makosa mengine kama vile ubadhirifu hayakuelezwa vizuri kwenye sheria ya zamani lakini hivi sasa makosa mengi yanaingia kwenye sheria mpya,” alisema.


Aliongeza kuwa awali taasisi hiyo ilishughulikia makosa manne tu ambayo ni kutoa na kupokea rushwa, matumizi ya nyaraka kupotosha, kutumia mamlaka kujinufaisha na ulimbikizaji wa mali lakini katika sheria mpya kuna makosa 24 yanashughulikiwa.


Alisema Takukuru inaandaa utaratibu wa kutoa mafunzo kwa waandishi wa habari kuhusu sheria mpya ya rushwa kwa kuwa wao wana mchango mkubwa katika kupambana na rushwa.


Source: Habari Leo

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents