Habari

TANESCO kuiomba Serikali kupandisha gharama za umeme

SHIRIKA la Umeme Tanzania (TANESCO) lina mpango wa kuiomba Serikali kwa mara nyingine kupandisha gharama za malipo ya huduma za umeme kutokana na kubanwa na ukubwa wa gharama za uendeshaji huku ikikabiliwa na madeni makubwa.

Na Charles Mwakipesile, Mbeya

 

SHIRIKA la Umeme Tanzania (TANESCO) lina mpango wa kuiomba Serikali kwa mara nyingine kupandisha gharama za malipo ya huduma za umeme kutokana na kubanwa na ukubwa wa gharama za uendeshaji huku ikikabiliwa na madeni makubwa.

 

Hayo yalisemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika hilo, Dkt. Idrisa Rashid alipokuwa akizungumza na viongozi na wafanyakazi wa shirika hilo mjini hapa.

 

“Hali ya shirika si nzuri kutokana na gharama kubwa za uendeshaji na madeni makubwa tunayodaiwa ambapo ili kufikia lengo letu, hata sasa tunatarajia kuiomba Serikali kwa mara nyinginetuongeze kodi zetu zetu kwani hizi za sasa ni ndogo ukilinganisha na bei ya umeme tunayonunua,”alisema

 

Katika mada yake ya mwelekeo na mipango ya shirika hilo iliyochukua saa tatu ,kiongozi huyo alisema kuwa hali ya shirika hilo ni mbaya kutokana na ukweli kuwa limegubikwa na matatizo makubwa ya ukata wa fedha hasa kutokana na Serikali kutangaza kufuta utaratibu wa kutoa ruzuku.

 

Alisema kutokana na hali hiyo kinachotakiwa ni mabadiliko makubwa ya kiuendeshaji ili kufikia lengo la kuondoa matatizo kwa wateja yanayotokana na ubovu wa miundo mbinu na uhaba wa vitendea kazi unaozua malalamiko mengi, samba samba na kukaribisha vitendo vya rushwa.

 

Dkt. Rashid alisema kuwa wakati wa kutaka kuendesha shirika hilo kisiasa umepitwa na wakati kutokana na ukweli kuwa liko katika hali mbaya ambayo kwa hakika kama haitarekebishwa ni wazi kuwa itaweza kusababisha madhara makubwa kwa uchumi wa nchi.

 

Alisema kuwa kazi kubwa iliyopo kwa wafanyakazi na viongozi wa shirika hilo ni kuhakikisha wanafanya kazi kubwa itakayowezesha kufanikiwa kwa shughuli nzima la uinuaji wa mapato ya shirika hilo na kuachana na tabia ambazo zilichangia kufikia hali hiyo mbaya ambayo kila mtu hatamani kuiona wala kuisikia.

 

Akiendelea kufafanua hoja hiyo, iliyokuwa imetokana na maswali ya waandishi wa habari alisema kuwa ni kweli kuwa hali ya kupanda kwa malipo ya huduma hiyo muhimu inaathiri upande wa wananchi wenye kipato cha kawaida ambapo hata hivyo kwa sasa hawana jinsi ya kukwepa.

 

Alisema kuwa Serikali baada ya kuona jinsi ambavyo shirika hilo lilikuwa likifanya biashara isiyo na faida, iliamua kusimamisha ruzuku kwa shirika hilo, hivyo kufanya kazi kubwa ya kuendesha shirika hilo kubaki mikononi mwa shirika.

 

Alisema kuwa kamwe maisha bora kwa kila Mtanzania hayatapatikana kama Watanzania watakuwa wanategemea kupata huduma hiyo bila kutambua kuwa ni gharama kubwa kuipata na kumudu uendeshaji wa mitambo na ununuzi wa umeme.

 

Bw. Rashid alisema alisema lengo lake ni kuona matatizo yaliyopo katika shirika hilo yanakwisha kwa kupatiwa ufumbuzi kwa kushirikiana na Watanzania wote.

 

Souce: Majira

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents