Habari

Tanesco wageuziwa kibao

MVUTANO kati ya Kampuni ya Saruji Tanga na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kuhusu malipo ya ankara ambao wiki iliyopita ulichangia Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo, Dk Idris Rashid, atangaze kujiuzulu, umeingia hatua mpya baada ya kampuni hiyo ya Tanga kusema itafungua kesi dhidi ya Tanesco, kwa kile inachodai ni kupakwa matope na kudhalilishwa na Menejimenti ya shirika hilo.

Mwandishi wa Habari Leo


MVUTANO kati ya Kampuni ya Saruji Tanga na Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) kuhusu malipo ya ankara ambao wiki iliyopita ulichangia Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo, Dk Idris Rashid, atangaze kujiuzulu, umeingia hatua mpya baada ya kampuni hiyo ya Tanga kusema itafungua kesi dhidi ya Tanesco, kwa kile inachodai ni kupakwa matope na kudhalilishwa na Menejimenti ya shirika hilo.


Mjumbe wa Bodi ya Wakurugenzi wa kiwanda hicho, Profesa Samwel Wangwe, alisema Dar es Salaam jana kwamba madai ambayo yamekuwa yakitolewa na Tanesco kuwa kiwanda hicho kilipitisha pembeni umeme ili kisilipe gharama sio ya kweli na yameifanya ionekane mbele ya jamii kuwa ni ya kihuni.


“Kwa kweli taarifa ambayo Tanesco wameitoa jana (juzi) imefanya tuonekane sisi kama sio wastaarabu mbele ya jamii. Hali hii inatishia uhusiano wetu na Tanesco, ndiyo maana tunaona tuchukue hatua za kisheria kama njia ya kujisafisha,” alisema Profesa Wangwe, aliyekuwa anazungumza kwa niaba ya Mwenyekiti wa bodi ya kiwanda hicho Dave King.


Alisema kilichokuwapo ni tatizo la moja ya kifaa ambacho kiwanda hicho kiliutaarifu uongozi wa Tanesco na sio kwamba kiwanda hicho kiliwahi kushindwa kulipa deni, “Kwa nini waseme sisi wezi…kwa kweli hatutaki kuonekana sisi ni kampuni ya kihuni.”


Profesa Wangwe alisema baada ya mvutano kati ya kiwanda na Tanesco juu ya gharama sahihi zilizotakiwa kulipwa katika kipindi cha siku tatu ambazo umeme haukupitia katika mita, Jumatano wiki hii kiwanda hicho kililipa Sh milioni 49 na adhabu ya Sh milioni 6.6 ambazo zililipwa kwa hundi.


“Sisi kama wawekezaji na tukiwa moja ya wateja wakubwa wa Tanesco tumesikitishwa na kauli iliyotolewa na menejimenti ya Tanesco jana (juzi) katika mkutano wake na waandishi wa habari ambayo imetuchafua,” alisema .


Alisema malipo hayo wameyafanya katika kipindi ambacho Tanesco waliwataka kuwa wamelipa na jana wamepokea barua kutoka Tanesco wakikiri kuwa wamepokea malipo hayo ndani ya kipindi ambacho walitakiwa kufanya hivyo.


“Lakini hakuna dalili kwa Tanesco kusahihisha taarifa yao waliyoitoa kwa umma jana,” alisema Wangwe na kuongeza kuwa wao kama mojawapo ya wateja wakubwa wa shirika hilo wanashangazwa na kauli za menejimenti hiyo.


Alisema wakati kuna matatizo ya umeme kiwandani hapo, wamekuwa wanafanya kazi kwa karibu katika kushughulikia matatizo ya umeme yanayokikabili kiwanda hicho, “Lakini tunashangazwa wenzetu wametugeuka, wanadai tumechezea umeme.”


Kampuni ya Tanga inadai kuwa kila mwezi inalipa Sh milioni 450 kama gharama za umeme na licha ya matatizo ya kukatikakwa umeme kiwandani hapo, hali iliyosababisha hasara ya Sh bilioni mbili hawakuwahi kudai fidia yoyote kutoka Tanesco.


Akielezea matatizo ya umeme kiwandani hapo, Wangwe alimtaja meneja wa usambazaji wa Tanesco, William Mhando, kuwa ndiye ambaye alitaarifiwa tatizo la kifaa hicho. “Tulimtaarifu tatizo la kifaa hicho kuwa kinatakiwa kibadilishwe, lakini licha ya kuahidi kufanya hivyo hakutokea.


Alisema sio kosa la kiwanda hicho kuhusiana na kifaa hicho, kwani Tanesco yenyewe haikuchukua hatua za haraka za kukibadilisha, hali iliyosababisha kutokea kwa matatizo ya kukatiwa umeme, kwa madai kuwa kilipitisha umeme nje ya mita.


“Kila siku walikuwa wanatupiga tarehe kuwa watakuja kubadilisha kifaa hicho, lakini leo hii sisi tumekiondoa ili kuiba umeme wakati hakukuwa na mawasiliano mazuri miongoni mwa Tanesco wenyewe,” alisema.
Menejimenti ya kiwanda hicho imemlaumu Mkurugenzi Mtendaji wa Tanesco, Dk Idris Rashid, ikidai kuwa baada ya kutokea matatizo ya umeme katika kiwanda hicho walijaribu kumpigia simu mara 50, lakini hakupokea.


Source: Habari Leo

Related Articles

Check Also
Close
Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents