Habari

Tanzania yakopeshwa Tsh. Trilioni 1 na Benki ya Dunia

Benki ya Dunia imeipatia Tanzania mkopo wenye masharti nafuu wa dola za Marekani milioni 450 sawa na shilingi za Tanzania trilioni 1.035, kwa ajili ya utekelezaji wa Awamu ya Pili ya mpango wa kunusuru kaya masikini unaotekelezwa na Mfumo wa Maendeleo ya Jamii- TASAF, awamu ya tatu.

Tukio hilo limefanyika Jijini Dar es Salaam kati ya Katibu Mkuu-Hazina Bw. Doto James na Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia Bi. Bella Bird.

Bw. James amesema hatua hiyo imefikiwa baada ya kupatikana kwa mafanikio makubwa ya awamu mbili zilizopita kwa kusaidia kaya masikini kwa kuongeza kipato na huduma za kijamii, kiuchumi ikiwemo kuwaendeleza watoto wao.

“Mpango huu katika kipindi cha pili ni kuwezesha kaya masikini kutumia fursa ya kuongeza kipato na huduma za kijamii na kiuchumi na kuwekeza katika maendeleo ya watoto wao” alisema Bw. James

Alisema malengo mengine yatakuwa ni kutekeleza miradi inayotoa ajira za muda ikihusisha ujenzi wa miundombinu hususan kwenye sekta mahususi kamavile afya, elimu, maji, kuimarisha taasisi na mifumo.

“Awamu hii ya pili inakwenda sambamba na Mpango wa Taifa wa Maendeleo wa Miaka Mitano, Mkakati wa Kukuza Uchumi na na Kupunguza Umasikini Zanzibar (MKUZA) utakao iwezesha Tanzania kufikia uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025” aliongeza Bw. James

Katika hafla hiyo Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Ikulu ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Mfuko wa Maendeleo ya Jamii TASAF Dkt. Moses Kusiluka, alisema kuwa kaya masikini watumie fursa hii kwa kuongeza kipato na huduma za jamii kwa lengo la kupunguza umasikini uliokithiri.

Alisema nia njema ya Mhe. Rais Dkt. John Pombe Magufuli ya kuwajali wanyonge na kwa kupitia fedha hizo anaamini jamii itanufaika na ameahidi kuzisimamia fedha hizo kikamilifu ili zitumike kwa malengo yaliyokusudiwa.

Alisema TASAF itahakikisha kuwa kaya zinazoishi katika umasikini uliokithiri zinapata stadi na elimu ya utunzaji wa fedha na hatimaye kupata fursa ya kukopa katika taasisi mbalimbali za fedha na hivyo kukuza uchumi wa kaya zao na kujenga rasilimali watu hasa watoto wanaohudhuria kliniki na wale walioko shuleni ambao wanaishi katika mazingira magumu.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkazi wa Benki ya Dunia Bi. Bella Bird amesema Benki yake imefurahishwa na namna Serikali ya Tanzania kwa usimamizi mzuri wa fedha na  ilivyotekeleza kwa ufanisi mpango huo wa kunusuru kaya masikini katika awamu zote za uwepo wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii TASAF

Alisema kuwa kupitia fedha hizo, jamii itaimarisha lishe, maisha ya watu na kuongeza mahudhurio ya wanafunzi wa shule za msingi na Sekondari darasani pamoja na huduma za afya.

Kwa upande wake Katibu Mkuu kutoka Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, Bw. Shaaban Mohamed, ameishukuru Benki ya Dunia kwa kutoa mkopo huo wenye masharti nafuu na kueleza kuwa Zanzinbar imekuwa mnufaikaji mkubwa wa mpango huo wa kunusuru Kaya Masikini.

Mwaka 2000, Serikali ilianzisha Mfumo wa Maendeleo ya jamii –TASAF kwa madhumuni ya kusaidiana na vyombo vingine vya Serikali kupunguza umasikini. Awamu ya kwanza (TASAF I) ilitekelezwa mwaka 2000 – 2005 ambapo jumla ya miradi ya kijamii 1,704 yenye thamani ya shilingi bilioni 72 ilitekelezwa ikiwemo ujenzi wa madarasa, miundombinu ya umwagiliaji pamoja na mabwawa ya kuhifadhi maji wakati wa mvua, ujenzi wa barabara vijijini, vituo vya afya, nyumba za walimu kwenye Halmashauri 40 za Tanzania Bara na Zanzibar.

Mwaka 2005 – 2013 awamu ya pili (TASAF II) ilitekeleza miradi ya kijamii 12,347 yenye thamani ya shilingi bilioni 430 katika Halmashauri 126 za Tanzania Bara, Unguja na Pemba, na kuwanufaisha watu 18,682,208.

“Mafanikio yaliyopatikana katika awamu zote mbili imepelekea Serikali kutekeleza awamu ya tatu (TASAF III) mwaka 2012, ambayo itatekelezwa kwa miaka 10 mpaka 2023 katika vipindi viwili ambapo kipindi cha kwanza kitafikia ukomo mwaka huu 2019, na Awamu ya Pili ambayo mkatabata wa mkopo umesainiwa, utakamilika mwaka mwaka 2023.

Related Articles

Back to top button

Adblock Detected

Please don't block our ads, we rely on these ads to serve you with credible contents